Urusi na Marekani kufanya mazungumzo bila ya Ukraine
18 Februari 2025Marekani na Urusi zimekubaliana mjini Riyadh kuendelea na juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Tammy Bruce amesema pande hizo mbili zilikubaliana kuteuwa timu za ngazi ya juu ili kuanza kufanya kazi ya kumaliza mzozo wa Ukraine haraka iwezekanavyo, kwa njia ya kudumu, endelevu na inayokubalika na pande zote.
Ujumbe wa Marekani uliongozwa na waziri wa mambo ya nje Marco Rubio wakati waziri mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov akiiwakilisha Urusi. Rubio amesema kumaliza vita vya Ukraine kutahitaji makubaliano kutoka pande zote
"Nadhani diplomasia inategemea vitendo, inatokana na ahadi ambazo huwekwa. Kwa hivyo nimetoka leo kwenye kikao nikiwa na uhakika kwamba Urusi iko tayari kuanza kushiriki katika mchakato mzito wa kuamua jinsi gani na kwa haraka na kwa njia gani vita hivi vinaweza kumalizwa."
Ukraine haikushirikishwa katika mazungumzo hayo ya Riyadh. Viongozi wa Ukraine na Umoja wa Ulaya wana wasiwasi kwamba Rais Donald Trump anaweza kufikia makubaliano ya haraka na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambayo yanapuuza masilahi yao ya kiusalama, kuituza Moscow kwa uvamizi wake na kumwacha Putin kuwa huru kutishia Ukraine au nchi zingine katika siku zijazo.