Urusi: Mashambulizi ndani ya Ukraine ni ya "kulipa kisasi"
27 Mei 2025Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema Moscow iliamua kuyalenga "maeneo ya kijeshi" ya Ukraine kujibu mkururo wa mashambulizi yaliyofanywa na utawala mjini Kyiv ndani ya Urusi.
Taarifa hiyo imesema katika kipindi cha siku saba zilizopita, Ukraine ilirusha maelfu ya droni kuyalenga maeneo ya ndani ya Urusi ikiwemo ambayo hayana shughuli zozote za kijeshi.
Takwimu za wizara hiyo zinaonesha mifumo ya ulinzi ya Urusi ilidungua droni 2,331 zilizorushwa na Ukraine kati ya Mei 20 hadi leo Mei 27.
Urusi imeyatuhumu mataifa ya Ulaya kuichochea Ukraine kufanya mashambulizi ndani ya ardhi yake ambayo Moscow inasema hayaoneshi dhamira ya kweli ya kumaliza mapigano.
Katika mfululizo wa mashambulizi kuanzia siku Jumapili Moscow iliyalenga maeneo chungunzima ndani ya Ukraine na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 13.
Lavrov asema Trump ameonesha fadhaa kwa kumwita Putin "mwendawazimu
Hujuma hizo zilizusha hasira na ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa Ukraine na Ulaya huku Rais Donald Trump wa Marekani alikwenda mbali zaidi na kumshambulia mwenzake wa Urusi Vladimir Putin akisema "amegueka mwendawazimu" kwa kufanya mauaji ya watu yasiyo na ulazima.
Trump pia alitishia kuiwekea vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi Urusi iwapo itaendelea na vita badala ya kusaka amani.
Hii leo Jumanne, Waziri wa Mambo ya nchi za nje ya Urusi Sergei Lavrov, amesema Trump ametoa matamshi hayo katika kuonesha hisia kwa sababu anaona juhudi zake za kutafuta amani kwa ajili ya Ukraine zinahujumiwa na wanasiasa wa Ulaya.
''Rais Trump ni mtu anayependa kuona matokeo, na pale anaposhuhudia kundi dogo la wawakilishi wa Ulaya wanaanza kuhujumu jitihada zake kwa kuisukuma Ukraine ifanye matendo ya ajabu kama kuilenga Moscow kwa droni na miji mingine, na mashambulizi ya kuilenga helikopta ya Rais wa Urusi, bila shaka ataonesha aina fulani ya fadhaa na hasira.".
Lavrov alikuwa akizungumza baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan anayeitembelea Moscow.
Urusi na Ulaya zatumbukia kwenye mvutano mpya kuhusu Ukraine
Kwenye mkutano wao na waandishi habari, Lavrov amesema Urusi iko tayari kurejea mezani kwa mazungumzo na Ukraine pale pande zote mbili zitakapowasilisha mapendekezo yao kuhusu mwelekeo wa mazungumzo hayo.
Amesema hivi sasa Urusi inaandaa rasimu yake ya mapendekezo na pia nchi hiyo imekataa makao makuu ya kanisa katoliki duniani kuwa eneo jipya ya mazungumzo yajayo ya amani.
Lavrov amesisitiza Urusi bado inaamini Uturuki, imekuwa mwenyeji wa duru kadhaa za mazungumzo akti ya pande hizo mbili inafaa kuendelea na jukumu hilo.
Hayo yanajiri katika wakati mvutano mpya umeibuka kati ya Urusi na nchi za Ulaya hasa baada ya Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani kusema nchi za Ulaya zinazoiunga mkono Ukraine zimeiondolea zuio la kutumia makombora yake ya masafa Ukraine na kwamba sasa nchi hiyo inaweza kushambulia ndani ya Urusi.
Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema uamuzi huo ni wa "hatari na unakwenda kinyume na juhudi za kutafuta amani."