Urusi: Marekani ina jukumu muhimu kumaliza vita na Ukraine
17 Mei 2025Matangazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov amezungumza kwa njia ya simu leo Jumamosi na mwenzake wa Marekani Marco Rubio na kupongeza jukumu muhimu la Marekani katika kusaidia kufanikisha mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi pia imechapisha taarifa katika mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba Lavrov amekubaliana na Rubio kuendeleza mawasiliano kati ya Moscow na Washington.
Hayo yanajiri siku moja baada ya wawakilishi wa Urusi na Ukraine kufanya mazungumzo yao ya kwanza ya moja kwa moja ya amani huko Uturuki, baada ya miaka kadhaa ya kutofanikiwa kufikia makubaliano ya usitishaji mapigano. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, mataifa hayo mawili yameendelea kushambuliana.