Mvutano kati ya Harvard na utawala wa Trump wafikia patamu!
16 Aprili 2025Chuo Kikuu cha Harvardkimekuwa taasisi ya kwanza mashuhuri ya elimu ya juu nchini Marekani kupinga hadharani masharti mapya ya serikali ya Rais Donald Trump yanayolenga kuzuia maandamano ya wanafunzi na kusitisha programu za utofauti na ujumuishaji. Katika barua kali iliyoandikwa na mawakili wake, Harvard ilisema kuwa hatua hizo ni kinyume cha Katiba ya Marekani na haki za kimsingi za uhuru wa kujieleza.
Kwa majibu ya hatua hiyo, serikali ya Trump ilitangaza kusitisha zaidi ya dola bilioni 2.2 za ruzuku na mikataba ya serikali kwa Harvard, ikiifanya taasisi hiyo kuwa ya saba kupokonywa ufadhili miongoni mwa vyuo vikuu vya juu nchini humo—sita kati yake vikiwa vya Ivy League. Hatua hii imezua mvutano mkubwa unaoweza kufungua mlango kwa kesi kubwa ya kikatiba.
Katika taarifa yake, Rais wa Harvard, Alan Garber, alisema kuwa hakuna serikali — iwe ya mrengo wowote — inapaswa kuwa na uwezo wa kuamua nini cha kufundishwa, nani wa kuajiri au kujiunga na chuo, au maeneo yapi ya utafiti yazingatiwe. Alisisitiza kuwa Harvard haiwezi kukubali kuingiliwa kwa uhuru wake wa kitaaluma.
Uhuru wa vyuo na madai ya kisiasa
Serikali ya Trump imekuwa ikishinikiza vyuo vikuu kufuata ajenda zake kisiasa, hasa baada ya maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Wapalestina kufuatia mashambulizi ya mwaka 2023. Trump na maafisa wake wamevituhumu vyuo vikuu kusambaza chuki dhidi ya Wayahudi, nadharia za Kimarxi, na fikra kali za mrengo wa kushoto, wakitaka vyuo hivyo viwaadhibu waandamanaji na kuvifanyia ukaguzi.
Masharti mengine ya serikali kwa Harvard ni pamoja na kuacha kutumia vigezo vya rangi, asili au jinsia katika ajira na uandikishaji, pamoja na kukomesha programu zote za utofauti, usawa na ujumuishaji (DEI). Harvard imesema masharti hayo si ya kisheria na yanakiuka Sheria ya Haki za Kiraia.
Soma pia: Baada ya Harvard kukataa kuburuzwa, Trump aongeza vitisho
Licha ya kuwa na hazina ya msaada ya dola bilioni 53, ambayo ni kubwa kuliko ya chuo chochote Marekani, Harvard bado hutegemea ufadhili wa serikali kwa tafiti za kisayansi na kimatibabu. Ikiwa serikali itaendelea kuzuwia fedha hizo, chuo hicho huenda kikaingia katika hali ya kifedha ya kubana matumizi au kukata baadhi ya miradi.
Vyuo vingine vya kifahari kama Columbia, Princeton na Stanford vimeonyesha kuunga mkono msimamo wa Harvard. Rais wa muda wa Columbia, Claire Shipman, alisema kuwa baadhi ya masharti ya serikali "hayakubaliki hata kidogo," na akasisitiza kuwa chuo chake kitahakikisha uhuru wa kitaaluma unalindwa.
Mgogoro unaohatarisha uhusiano wa miaka
Mgogoro huu unaonekana kuathiri moja ya uhusiano wa muda mrefu kati ya serikali ya shirikisho na vyuo vikuu binafsi—ambapo kwa miongo kadhaa, serikali imekuwa ikisaidia vyuo kupitia ruzuku kwa ajili ya tafiti na maendeleo. Sasa, fedha hizo zimegeuzwa kuwa chombo cha shinikizo la kisiasa.
Wachambuzi wanasema huenda kesi kubwa ya kisheria ikafunguliwa iwapo mvutano huu utaendelea. Tayari kundi la wahadhiri limeshafungua kesi dhidi ya serikali likidai masharti hayo yanakiuka haki za uhuru wa kujieleza na mchakato wa haki. Wengi pia wanatarajia Harvard yenyewe ifungue kesi yake.
Soma pia: Havard yamtunukia Merkel Shahada ya Udaktari wa Heshima
Rais wa zamani Barack Obama ameunga mkono hatua ya Harvard, akisema kuwa imekataa "jaribio la serikali la kutumia nguvu kuua uhuru wa kitaaluma.” Wanafunzi wengine wa vyuo vingine wameanza kueleza msimamo wao hadharani, huku baadhi wakihamasisha kujitokeza kwa maandamano ya kuunga mkono uhuru wa elimu.
Huku hali ya kisiasa ikizidi kupamba moto kuelekea uchaguzi wa 2026, Harvard imekuwa mfano wa taasisi inayosimama kidete kupinga kile kinachoonekana kuwa jaribio la serikali kudhibiti taasisi binafsi kwa kutumia ufadhili kama fimbo ya kisiasa. Swali linalosalia ni: Je, vita vya kisheria vinaweza kuleta mabadiliko au vitaongeza mgawanyiko zaidi katika mfumo wa elimu wa Marekani?