Upinzani Sudan Kusini walia na kamatakamta dhidi ya viongozi
26 Machi 2025Chama cha upinzani nchini Sudan Kusini, SPLM-IO, kimesema kuwa viongozi wake kadhaa muhimu wamekamatwa, siku moja tu baada ya kambi yake ya kijeshi kushambuliwa karibu na mji mkuu, Juba. Mashambulizi hayo yameongeza wasiwasi mkubwa wa kurejea tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mzozo huu mpya unatokana na mvutano kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Riek Machar, na unatishia kuvunja makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2018. Uganda tayari imetuma vikosi mjini Juba, hatua ambayo chama cha Machar kimeilaani vikali, kikisema kuwa ni ukiukaji wa marufuku ya silaha iliyowekwa na Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Mjumbe wa UN aonya kuhusu hatari ya Sudani Kusini kurudi vitani
Chama cha SPLM-IO kimeripoti kuwa maafisa wake wanne, akiwemo Waziri wa Rasilimali za Wanyama na Uvuvi, Gai Magok, wamekamatwa katika kile kinachoelezwa kama kampeni pana ya serikali dhidi ya upinzani.
Hadi sasa serikali haijatoa kauli yoyote kuhusu madai hayo ya kukamatwa kwa viongozi wa upinzani.