Uongozi wa AU: Nani anaweza kutatua changamoto za Afrika?
15 Februari 2025Kadiri Umoja wa Afrika (UA) unavyojiandaa kuchagua mwenyekiti wake mpya wa tume mwezi Februari, wagombea watatu wakuu wako kwenye mwangaza wa kujaza kiti hicho cha juu cha kidiplomasia barani Afrika.
Mmoja wao ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf, mwanadiplomasia mwenye uzoefu anayejua jinsi ya kupenya katika vichochoro vya madaraka. Anashindana na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato, mchumi anayewania kubadilisha taswira ya bara zima.
Lakini anayeongoza katika mbio hizi ni gwiji wa siasa wa Kenya, Raila Odinga, mpiganaji wa kisiasa ambaye bado anahitajika kushughulikia mapambano yake ambayo hayajakamilika nyumbani.
Kila mmoja kati ya hawa ana mtazamo tofauti kuhusu bara la Afrika, na kila mmoja anadai kuwa na uzoefu unaohitajika kwa kazi hiyo. Lakini ni nani kati yao anayeweza kweli kusema ana kile kinachohitajika kuiongoza Afrika katika sura yake inayofuata?
Urithi wa Odinga: Mgawanyiko Kenya lakini kuungwa mkono Afrika
Odinga ni mmoja wa wanasiasa wanaotambulika zaidi nchini Kenya—jina lake linachochea hisia kali za mapenzi na mgawanyiko kwa kiwango sawa.
Akiwa waziri mkuu wa zamani, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 80 anachukuliwa kuwa bingwa wa demokrasia asiyeogopa na wafuasi wake. Kwa wakosoaji wake, hata hivyo, yeye ni kama kisiki cha zamani cha siasa: mgombea wa urais mara tano aliyebobea katika kushindwa na kukataa kufifia kisiasa.
Soma pia: Afrika kumchagua mwenyekiti wa AU
Ingawa Odinga amepata changamoto kushawishi wapiga kura wa Kenya, uzoefu wake katika mazungumzo ya amani na maendeleo ya miundombinu barani Afrika umempa heshima nje ya mipaka ya nchi yake.
Katika wadhifa wake kama Mwakilishi Maalum wa AU wa Miundombinu, alishinikiza miradi mikubwa kama vile Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na uanzishwaji wa njia za usafiri za kikanda.
Lakini je, anaweza kuiongoza AU wakati nchi yake yenyewe bado ina mashaka kuhusu uongozi wake?
Asiyependwa na Vijana wa Kenya
Wakosoaji wake wa ndani wanadai kuwa uhusiano wake wa karibu na tawala za zamani za Kenya na makubaliano yake ya hivi karibuni na Rais William Ruto—hata kama ni kwa shingo upande—unaonyesha kuwa anajali zaidi maisha yake ya kisiasa kuliko kutoa uongozi wa mabadiliko ya kweli.
Katika mitaa ya Nairobi, maoni kuhusu Odinga yanatofautiana zaidi ya hapo awali.
"Nadhani umaarufu wake umepungua, na kufikia kiwango cha chini kabisa mwaka jana wakati wa maandamano dhidi ya Muswada wa Fedha," anasema Eugene Omar, mtaalamu wa programu wa Kenya, alipoulizwa kuhusu mtazamo wake kwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 80.
Omar pia alimwambia DW kuwa anahisi Odinga ameacha kuwasikiliza wananchi, hasa vijana wa Kenya, ambao wanashiriki mashaka yake kuhusu azma ya Odinga ya kuongoza AU.
Soma pia:Umoja wa Afrika 'wasikitishwa' na Marekani kujiondoa WHO
"Watu walihisi kusalitiwa sana kwamba alijiunga na upande wa Rais Ruto, ilhali vijana wengi nchini waliona ni wakati wa mabadiliko. Kwa hivyo, kwa sasa, sijui ni kwa nini anaonekana kuwa maarufu kwa kiti cha AU, ilhali watu wengi wa nchi yake hawaamini uongozi wake."
Kwa kweli, idadi kubwa ya Wakenya wanasema wanapinga azma ya Odinga, huku baadhi, kama mtaalamu wa vyombo vya habari Keit Silale, wakiamini bado ndiye mtu sahihi kwa kazi hiyo.
"Uzoefu wake mkubwa katika utawala na diplomasia, ikiwemo nyadhifa zake za awali kama Mwakilishi Maalum wa AU kwa Maendeleo ya Miundombinu, unamuweka katika nafasi nzuri ya kushughulikia changamoto za bara," aliiambia DW.
"Uwezo wake wa kuongoza katika mazingira tata ya kisiasa pia unaweza kuwa na manufaa katika kutatua changamoto kuu za bara hili."
Youssouf: Diplomasia kama nguvu na msingi
Akiwa na umri wa miaka 59, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf, ni miongo miwili mdogo kuliko Odinga, na amekuwa mwanadiplomasia mkuu wa nchi yake kwa muda mrefu kama huo.
Youssouf analeta uelewa wa kina wa jiografia ya kisiasa ya Afrika katika kinyang'anyiro hiki: Kuanzia usuluhishi wa amani katika Pembe ya Afrika hadi kusawazisha uhusiano na mataifa makubwa duniani, ameiweka nchi yake kama mhimili muhimu wa bara na kwingineko.
Dira yake kwa AU ni kabambe: sera madhubuti za usalama, muungano wa kikanda wenye nguvu, na Afrika yenye msimamo thabiti katika jukwaa la kimataifa.
Uzoefu wake unajumuisha kuandaa mikataba na mataifa yenye nguvu huku akihakikisha kwamba Djibouti inabaki kuwa eneo la kimkakati kwa majeshi ya mataifa makubwa.
Hii ndiyo sababu iliyopelekea mfanyabiashara wa benki wa Kenya, Kevin Sewe, kumpendelea Youssouf badala ya Odinga.
"Nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye nguvu, kijana, mtu ambaye anaweza kusafiri kote barani kutoka Sahel hadi Sudan hadi DRC, kwa hivyo ninaona yule Djiboutian ana nafasi bora zaidi," Sewe aliambia DW.
Soma pia:Kenya yaunda kamati ya ushindi ya Odinga
Hata hivyo, wakosoaji wanasema rekodi ya Djibouti kuhusu haki za binadamu na ukosefu wa demokrasia vinaweza kuwa vizuizi kwa Youssouf.
Djibouti imekuwa ikitawaliwa na Rais Ismail Omar Guelleh tangu 1999 bila upinzani mkubwa wa kisiasa, jambo linalowafanya wengi kujiuliza ikiwa Youssouf ataleta uhuru wa kutosha kuiongoza taasisi kuu ya Afrika badala ya kutanguliza maslahi ya serikali yake.
Randriamandrato: Uchumi Pekee Ndio Unaoweza Kuirekebisha Afrika
Akiwa na umri wa miaka 56, Richard Randriamandrato ndiye mgombea mwenye umri mdogo zaidi katika kinyang’anyiro hiki. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Madagascar ni mchumi kitaaluma na si mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa.
Lakini Randriamandrato anaamini kwamba takwimu, si hotuba za kisiasa, ndizo zinaweza kufungua uwezo wa Afrika.
Anaona AU inayoendeshwa na uhuru wa kifedha, biashara ya kikanda, na maendeleo endelevu badala ya mivutano ya kidiplomasia isiyo na mwisho.
Lakini je, utaalamu wake unatosha kumpa nafasi ya kuongoza? Wengi wanahoji kuwa hana uzoefu wa kisiasa na kidiplomasia unaohitajika kwa kazi hiyo.
Nani Ataweza Kutatua Changamoto za Afrika?
Katika mchakato wa kuchagua mwenyekiti mpya wa AU, nchi wanachama zitapaswa kuzingatia ni sifa gani muhimu zaidi kwa nafasi hiyo: ushawishi wa kisiasa, ujuzi wa kidiplomasia, au mtazamo wa kiuchumi wa kimapinduzi?
Soma pia:Wagombea wa uenyekiti wa tume ya AU washiriki katika mdahalo
Mwenyekiti ajaye wa AU atapaswa kukabili changamoto kubwa kama vita Sudan na DRC, tawala za kijeshi Afrika Magharibi, mdororo wa uchumi, na mabadiliko ya tabianchi.
Je, Afrika itamchagua mwanasiasa mwenye uzoefu, mwanadiplomasia mahiri, au mchumi shupavu? Jibu litasubiriwa Addis Ababa.