UNICEF yaonya kuhusu hali ya watoto katika Ukanda wa Gaza
5 Septemba 2025Katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana, msemaji wa UNICEF, Tess Ingram, amesema mji wa Gaza City, kimbilio la mwisho kwa familia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, unaibuka kwa haraka kuwa mji wa hofu, uhamaji na mazishi.
Afisa huyo wa UNICEF amesema hali ilivyo katika eneo hilo la Palestina haikutokea kwa bahati mbaya ila ni matokeo ya moja kwa moja ya maamuzi ambayo yameligeuza Jiji la Gaza na Ukanda mzima wa Gaza kuwa mahali ambapo watu wanashambuliwa kutoka kila upande kila siku.
Kwa sasa, jeshi la Israel linajiandaa kuliteka Jiji la Gaza, ambao ndio mji mkubwa zaidi katika Ukanda huo. Maelfu ya askari wa akiba wa Israel waliitwa siku ya Jumanne.
Huku hayo yakijiri, maafisa wa afya wa Gaza wamesema mashambulizi ya Israel jana katika ukanda huo yamesababisha vifo vya takriban watu 53 wengi ndani ya Jiji la Gaza, ambapo vikosi vya Israel vimesonga mbele katika viunga vya mji huo na sasa viko umbali wa kilomita chache kutoka katikati mwa mji huo.
Msemaji wa jeshi hilo la Israel, Brigadia Jenerali Effie Defrin, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wataendelea kuharibu miundo mbinu ya Hamas na kwamba kwa sasa wanadhibiti asilimia 40 ya jiji hilo, akivitaja viunga vya Zeitoun na Sheikh Radwan.
Defrin amesema wataendelea kuliandama kundi la Hamaspopote pale na akongeza kuwa operesheni hiyo itamalizika tu wakati mateka wa Israel waliosalia watakaporejeshwa na utawala wa Hamas kusambaratishwa.
Waziri wa Uingereza atetea mkutano na Rais wa Israel
Katika hatua nyingine, waziri wa biashara wa Uingereza Douglas Alexander, ametetea uwezekano wa maafisa wa serikali ya nchi hiyo kukutana na Rais wa Israel Isaac Herzog wakati wa ziara yake nchini humo wiki ijayo huku kukiwa na ukosoaji wa ndani kutoka kwa maafisa wa serikali.
Alexander amesema Uingereza lazima ishirikiane na Israel pamoja na Mamlaka ya Palestina kama sehemu ya shinikizo la kidiplomasia la kumaliza vita katika ukanda wa Gaza.
Ziara ya kiongozi huyo wa Israel, katika wakati ambapo hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ni mbaya na Israel inasonga mbele kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi, imezua ghadhabu miongoni mwa baadhi ya wabunge nchini Uingereza.