UNHCR yaelezea wasiwasi kuhusu mgogoro nchini Kongo
14 Februari 2025Msemaji wa UNHCR Eujin Byun, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kwamba takriban wakimbizi 350,000 wa ndani hawana makazi kwasababu kambi zao za muda zimeharibiwa ama kuwepo kwa mabomu ambayo hayajaripuka kufanya kuwa hatari kwao kurudi nyumbani.
Wakimbizi wa ndani wanaishi makanisa na hospitalini
Kulingana na UNHCR, takriban asilimia 70 ya kambi katika eneo la Goma zimeharibiwa pamoja na nyingine huko Minova.
Moto na Ghadhabu: Vita vikali vya Goma, DRC
Byun ameongeza kuwa maelfu ya watu sasa wanaishi kwenye kambi za muda ikiwa ni pamoja na makanisa na hospitali.
Kundi la M23 lawaagiza wakimbizi Goma kuondoka kwenye kambi
Shirika la kutetea hali za binadamu Human Rights Watch limesema leo kuwa kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda limewaagiza maelfu ya wakimbizi wa ndani kuondoka kwenye kambi katika eneo la Goma mashariki mwa Kongo.
Mtafiti mkuu wa Afrika katika shirika hilo la Human Rights Watch Clementine de Montjoye, amesema kuwa agizo hilo la M23 la kuwaondoa kwa nguvu maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutoka kambini hadi maeneo ambayo hayana msaada ni la kikatili na lenye uwezekano wa kuwa uhalifu wa kivita.
Montjoye ameongeza kuwa Rwanda na nchi nyingine zenye ushawishi juu ya M23zinapaswa kushinikiza kundi hilo lililojihami kukomesha hatua hiyo mara moja.
Kundi la CODECO lafanya mashambulizi dhidi ya vijiji
Ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo MONUSCO, umesema jana kuwa zaidi ya raia 80 waliuawa kwenye shambulizi la usiku lililofanywa na wapiganaji wa kundi la CODECO dhidi ya vijiji kadhaa mashariki mwa Kongo wiki hii .
CODECO, moja ya makundi ya wapiganaji yanayopigania ardhi pamoja na raslimali nyingine, limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika kambi za wakimbizi wa ndani ambazo zimeongezeka tangu kuanza kwa mashambulizi ya kundi la M23.