UNHCR: Kupungua kwa ufadhili kunatishia maisha ya mamilioni
29 Machi 2025Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limelionya kwamba kupunguzwa kwa ufadhili katika shirika hilo, kunatishia afya ya karibu watu milioni 13 waliokimbia makazi yao.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu kote duniani yamekuwa yakiyumba tangu Rais waMarekani Donald Trump aliporejea madarakani mwezi Januari, akisukuma ajenda ya kupinga wakimbizi na wahamiaji huku akisitisha ufadhili wa Marekani kwenye mashirika hayo.
Soma zaidi: Guinea:Aliyekuwa kiongozi wa kijeshi asemehewa kwa mauaji
Mkuu wa afya ya umma wa UNHCR Allen Maina ametolea mfano katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwamba bajeti ya afya ya UNHCR ya mwaka 2025 imepunguzwa kwa asilimia 87 ikilinganishwa na mwaka 2024 na kuwaweka zaidi ya wakimbizi 520,000 katika hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukiza pamoja na vifo.
Nchini Burundi tayari programu za lishe katika kambi kadhaa za wakimbizi zimesimamishwa, hatua ambayo huenda ikapelekea maelfu ya watoto wakimbizi walio na umri wa chini ya miaka mitano kushindwa kupata matibabu ya kutosha kutokana na utapiamlo.