Unafahamu kuwa makengeza yanaweza kutibiwa?
19 Mei 2025Kwa mujibu wa Wizara ya Afya nchini Tanzania, nchi hiyo inakabiliwa na matatizo ya aina nyingi ya macho, na inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja wana changamoto za magonjwa ya macho. Veronica John Hitu, ni mama wa makamo ambaye amepata changamoto ya uoni hafifu kutokana na kubainika kuwa na ugonjwa wa makengeza.
''Tatizo lilianza tu sioni, nikishika karatasi kwa sababu mimi ni muuguzi kwa hiyo nilipokuwa kwenye kazi nilikuwa sioni zile karatasi nyeupe kama nasoma cheti. Kwa hiyo ikawa sioni kabisa. Nahisi kwangu mimi chanzo kilikuwa hicho. Kwa hiyo walivyonipima wakagundua nina shida kweli wakanipatia miwani,'' alifafanua Veronica.
Makengeza yanaweza kurithiwa pia
Ugonjwa wa makengeza, ni hali ya macho kutotazama sehemu moja kwa pamoja, kutokana na uumbwaji wa binadamu kuumbwa na macho mawili, ambayo mara zote kutazama upande mmoja kwa pamoja, lakini mtu anapokuwa na tatizo hilo la makengeza macho yake yanakuwa yanapishana katika kutazama kitu.
Tatizo hilo linaweza kubainika kwa mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa, au miaka miwili hadi mitatu baada ya kuzaliwa. kwa watoto wachanga. Tatizo hilo linaweza kutokea kwa sababu ya kuzaliwa njiti, au magonjwa ya kurithi, magonjwa ya kimaumbile, utindio wa ubongo, na kurithi kutoka kwa wazazi wake.
Shafii Suleimani Milela ni mtaalamu wa afya ya macho na uono kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara, anasema lakini pia mtoto anaweza akapata kengeza, muda mfupi baada ya kuzaliwa ikiwa macho yake mawili yana utofauti wa uono, ambapo jicho moja linakuwa limepungua zaidi nguvu ya kuona kuliko jicho lingine.
''Taarifa za uono za macho haya mawili zinazoenda kwenye ubongo zinakuwa zinatofautina na mara zote ubongo unapendelea ile taarifa ambayo ipo wazi zaidi. Kwa hiyo, ile taarifa ambayo inakuwa na changamoto kutoka kwenye jicho ambalo halioni vizuri inakuwa mara nyingi inapuuzwa na ubongo na kusababisha hili jicho kupinda, na linapopinda linasababisha kuwepo kwa kengeza,'' alibainisha mtaalamu huyo wa macho.
Watu wazima pia wanaweza kupata makengeza
Kadhalika Milela anasema watu wazima nao wana uwezekano wa kupata ugonjwa wa makengeza kutokana na kupata ajali iliyohusisha kuathiri sehemu ya kichwa, au kuugua ugonjwa wa kiharusi, inagawa ajali hiyo hiyo inaweza kusababisha changamoto kwenye kuvunjika sehumu ya kichwa, hususan sehemu ya mzingo wa jicho.
''Sehemu ile ya mfupa inakabana na msuli mmoja wapo, kwa hiyo ile inaweza kusababisha jicho likawa haliwezi kujongea, katika uwelekeo fulani, na matokeo yake yakatengeza kengeza, lakini ajali hiyo hiyo pia inaweza ikasababisha changamoto kwenye mishipa ya fahamu, na mishipa ya fahamu ambayo inaweza ikapata athari ni mshipa wa fahamu namba tatu na mshipa wa fahamu wa usoni ambayo katika matawi tofauti inadhibiti sehemu tofauti za misuli ya macho,'' alisema mtaalamu Milela.
Kulingana na mtaalamu huyo wa afya ya macho na uono, vipo viashiria mbalimbali vya kubaini tatizo la makengeza kwa mtoto kama macho kupishana wakati wa kutazama, na kwa watu wazima kupatwa na tatizo la kutoona vizuri au jicho mojawapo kuwa na uono hafifu, kuona taswira mbilimbili, kupata maumivu ya kichwa, kizunguzungu, na kushindwa kuchakata taarifa unazozitazama kwa usahihi. Hata hivyo, habari njema ni kwamba ugonjwa huo una tiba kwa watu wa rika zote, kutegemea na ukubwa wa tatizo.
''Kwa watoto baada ya kufanya vipimo vyote, tunaangalia uwezo wa kuona, lakini katika aina hiyo ya kengeza huwa tunarekebisha kwa uvaaji wa miwani, lakini mara nyingine makengeza haya kutokana na sababu labda ya misuli au mishipa ya fahamu kutokufanya kazi vizuri wanaenda kufanyiwa upasuaji,'' alisisitiza Milela.
Lakini kwa watu wazima kama ulizaliwa nalo au lilitokea kipindi cha udogoni, halafu umefikia umri wa utu uzima sasa unataka ulirekebishe kengeza, linarekebishika pia, lakini mara nyingi tutakuwa tunarekebisha tu muonekano kwamba jicho litarudi katika uwelekeo wake mzuri, lakini uono unaweza usiwe mzuri sana.
Iwapo hautatibu tatizo la makengeza kunaweza kusababisha kupata tatizo la jicho vivu na kumuondelea mhusika hali ya kujiamini, hivyo wazazi na walezi mnashauriwa kuwapeleka hospitali watoto wenu pindi mnapoona dalili za makengeza kwa sababu uwepo wa tatizo hilo unaweza pia kuwa sababu ya kutokea kwa matatizo mengine ya macho.