Umoja wa Mataifa wazindua mpango wa kuimarisha ufanisi
17 Machi 2025Mpango huo unahusu kuharakisha ufanisi na maboresho katika shirika hilo. Akiuzindua mpango huo wakati Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 80, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na upungufu wa rasilimali ndani ya umoja huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo unaoitwa UN 80 Guterres amesema, Lengo la mpango huo ni kuwasilisha mapendekezo kwa mataifa wanachama katika maeneo matatu.
Moja ni kutambua haraka ufanisi na maboresho ya namna shirika hilo linavyofanya kazi na pili ni kutathmini utekelezaji wa mamlaka lililopewa na nchi wanachama ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.
Suala jingine ni kufanya mapitio ya kina ya kimkakati, mabadiliko zaidi ya kimfumo na kurekebisha programu ili ziendane na mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Ameeleza kuwa katika nyakati hizi zisizotabirika na zenye mashaka Umoja wa Mataifa unahitajika kuliko kipindi kingine chochote. Guterres ameongeza kuwa, shirika lake na bajeti zinazotajwa ni masuala nyeti ya kufa na kupona kwa mamilioni ya watu kote duniani.
Soma zaidi: Guterres ahimiza kuwepo kwa mshikamano wa kimataifa
Zaidi amesema, "Umoja wa Mataifa unaweza kubadilika kuendana na mazingira. Tatizo ni kwa watu. Hapa namaanisha kama watu wengi zaidi watakufa kwa Ugonjwa wa UKIMWI au Kifua Kikuu.
Kama misaada ya kiutu kwa jamii zenye matatizo itayafanya maisha yao kuwa magumu zaidi na kuwa na madhara makubwa si tu kwa maana ya kuokoa maisha lakini kwa mtazamo wa aina za msingi za ustawi. Hilo ni suala ambalo hatuwezi kulirekebisha."
Guterres amefafanua kuwa, shirika lenye mfumo mpana na muhimu kama Umoja wa Mataifa halina budi kufanya uchunguzi wa ya mara kwa mara ili kutathmini utendaji wake kwa madhumuni ya kuyafikia malengo yake kwa ufanisi.
Ametanabaisha kwamba wakati Umoja wa Mataifa ukiadhimisha miaka 80 ni wakati sahihi wa kufanya juhudi zote katika kutambua umuhimu wa kuharakisha ufanisi wa shirika hilo.
Kucheleweshwa michango ya wanachama kwamisha UN
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza pia kuwa, moja ya changamoto kubwa ni kuwa kwa miaka saba iliyopita shirika hilo limekuwa likikabiliwa na ukwasi kwa sababu si nchi zote wanachama zinazotoa michango yao kikamilifu na pia wafadhili wengi hawatoi fedha kwa wakati.
Kulingana na mmoja wa wasemaji wa Umoja wa Mataifa, Marekani kwa mfano, ndiyo mchangiaji mkubwa katika bajeti ya shirika hilo ambapo inatoa asilimia 22 ya bajeti nzima. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Januari ilikuwa na malimbikizo ya dola bilioni 1.5.
Mfano mwingine ni China inayotambuliwa kama mchangiaji mkubwa wa pili kwa bajeti ya Umoja wa Mataifa na haikulipa michango yake ya mwaka 2024 kwa wakati hadi ilipofika mwishoni mwa mwezi Desemba.
Ugumu zaidi unaoukabili Umoja wa Mataifa unachangiwa zaidi na tangazo la Marekani la kusitisha karibu misaada yote ya kiutu ambayo ilifadhili kwa kiasi kikubwa programu za Umoja wa Mataifa na mashirika yake.
Kuna wasiwasi mkubwa kuwa Rais wa Marekani Donald Trump atapunguza michango kwa bajeti ya umoja huo kama alivyofanya katika awamu yake ya kwanza. Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema Programu iliyozinduliwa na shirika hilo haitokani na shinikizo jipya la Marekani.