UN yasema malengo ya kupunguza joto duniani hayatafikiwa
28 Mei 2025Hii ina maana dunia inatarajiwa kusalia katika viwango vya juu kabisa vya joto baada ya kushuhudiwa miaka miwili yenye joto kali zaidi katika mwaka wa 2023 na 2024. Haya ni kwa mujibu wa ripoti iliyochaopishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi - WMO.
Naibu katibu mkuu wa WMO Ko Barrett amesema dunia imekuwa na miaka 10 yenye fukuto kali kabisa kuwahi kushuhudiwa. Amesema kwa bahati mbaya ni kuwa ripoti hiyo ya WMO haitoi dalili zozote za ahueni katika miaka ijayo, na hii ina maana kwamba kutakuwa na athari mbaya zinazoongezeka kwa uchumi wa dunia, maisha yetu ya kila siku, mifumo yetu ya ikolojia na sayari yetu.
Makubaliano ya Mazingira ya Paris ya 2015 yalilenga kupunguza ongezeko la joto duniani hadi chini ya nyuzijoto 2 za celcius juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya kiviwanda -- na hadi nyuzijoto 1.5 za celcius ikiwezekana.