UN yapunguza ufadhili wa misaada kwa Yemen, DRC na Somalia
17 Mei 2025Mwezi Januari mwaka 2025, Umoja wa Mataifa uliwasilisha ombi la dola bilioni 2.4 ili kuwasaidia watu milioni 10.5 katika nchi ya Yemen iliyoharibiwa na vita, huku ukikadiria kuwa watu milioni 19.5 ndio wanaohitaji msaada.
Lakini kutokana na kupungua kwa ufadhili, shirika hilo la kimataifa na washirika wake wa misaada ya kibinadamu walianzisha vipaumbele vipya ili kuweza kuwasaidia angalau watu wenye uhitaji mkubwa.
Katika wiki za hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ulitangaza pia mabadiliko sawa na hayo katika mkakati wake nchini Ukraine na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkakati mpya wa kupunguzwa misaada ya UN
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Bi Stephanie Tremblay amesema kwa sasa mwelekeo nchini Yemen utakuwa kuwasaidia pekee watu milioni 8.8 kulingana na bajeti inayotarajiwa ya dola bilioni 1.4.
Katika nchi ya Somalia inayokabiliwa na vurugu, mpango wa awali wa dola bilioni 1.4 wa kuwasaidia watu milioni 4.6 pia umepunguzwa hadi dola milioni 367 kwa ajili ya watu milioni 1.3, akisisitiza kuwa hii haimaanishi kuwa kumekuwa na kupungua kwa mahitaji ya kibinadamu.
Bi Tremblay amesisitiza kuwa kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ufadhili kumelazimisha programu za misaada ya kibinadamu kupunguzwa na hivyo kuyaweka maisha ya mamilioni ya watu hatarini kote ulimwenguni.
"Kama ilivyo katika majanga mengine, matokeo yatakuwa mabaya. Ikiwa tutashindwa kutekeleza wajibu wetu, mamilioni ya watu watakabiliwa na njaa, kukosa maji safi, elimu, ulinzi na huduma nyingine muhimu," aliongeza msemaji huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanapunguza pia harakati zake za utendaji na idadi ya wafanyikazi kote ulimwenguni huku yakikabiliana na punguzo kubwa la michango kutoka kwa nchi wanachama, haswa Marekani tangu aliporejea madarakani kwa muhula wa pili rais Donald Trump.
Hayo yakiarifiwa, ripoti mpya iliyotolewa Ijumaa na Umoja wa Mataifa imesema kumeshuhudiwa ongezeko la uhaba wa chakula na utapiamlo kwa watoto katika kipindi cha miaka sita mfululizo, na hivyo kuwaathiri zaidi ya watu milioni 295 katika nchi na maeneo 53 kote duniani.
(Vyanzo: AFP, Reuters)