UN yapunguza msaada Kongo kutokana na matatizo ya kifedha
9 Mei 2025Mwezi Februari, Umoja wa Mataifa ulitoa ombi la karibu dola bilioni 2.5 kuwasaidia watu milioni 11 nchini Kongo mwaka huu badala ya milioni 21 ambao Umoja wa Mataifa unawaona kuwa wanahitaji msaada.
Ofisi ya masuala ya kibinaadamu - OCHA imesema imeweka vipaumbele vipya kwa sababu msaada unapungua na mahitaji yanaongezeka. OCHA imesema kwa kuwa ni msaada wa dola milioni 245pekee ambao umepokelewa kujibu ombi hilo hadi sasa, mpango huo mpya umebainisha "hatua za kuokoa maisha zitakazowasaidia watu milioni 6.8 walio hatarini zaidi kwa gharama ya dola bilioni 1.25 -- takriban nusu ya mahitaji ya mpango kamili."
Hatua hiyo ya kupunguzwa kwa misaada inajiri wakati mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa yakipunguza operesheni zao na idadi ya wafanyakazi kote ulimwenguni huku wafadhili wakipunguza bajeti, hasa Marekani chini ya Rais Donald Trump.