UN yapunguza misaada duniani baada ya ufadhili kupungua
17 Juni 2025Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Jumatatu kwamba inatafuta ufadhili wa dola bilioni 29 kwa mwaka huu, ikilinganishwa na dola bilioni 44 zilizoombwa hapo awali mwezi Desemba, hatua "iliyopewa kipaumbele sana".
UNHCR, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, lilisema baadaye Jumatatu kwamba litalazimika kusitisha ajira kwa watu 3,500, na kupunguza asilimia 30 ya gharama za wafanyikazi wake, huku ufadhili ukizidi kudidimia.
Kupunguzwa kwa ghafla kwa ufadhili wa Marekani kumekuwa na athari kubwa kwa misaada ya dharura, kampeni za chanjo, na usambazaji wa dawa za kupambana na UKIMWI. Nchi nyingine kuu wafadhili pia zimepunguza michango yao kutokana na mtazamo wa kiuchumi usio na uhakika.
"Ninatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, wakuu wa nchi, Maafisa Wakuu, watu binafsi, mashirika yasiyo ya serikali, kukutana wakati huu kwa kusaidia wahudumu wa kibinadamu wanapokabiliana na migogoro duniani kote. Kwa sababu hatujakata tamaa na wewe pia usikate tamaa. Kutochukua hatua ni chaguo ambalo tunaweza kukataa kulifanya. Kuna kiwango cha juu sana cha hatari kinachohusika."
"Kupunguzwa kwa ufadhili kwa njia ya kikatili hutuacha na chaguzi za kikatili. Tunachoomba ni asilimia moja tu ya kile mlichopangia kutumia mwaka jana kwa ajili ya vita," alisema mkuu wa OCHA Tom Fletcher kupitia taarifa.
Afrika pia imeathirika na mpango wa misaada
Kauli ya Fletcher inakuja wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wametoa ripoti ya pamoja ya onyo la mapema kubainisha kuwa Sudan, maeneo ya Palestina, Sudan Kusini, Haiti na Mali yana jamii ambazo "tayari zinakabiliwa na hatari ya njaa au kukabiliwa na viwango vya janga la uhaba mkubwa wa chakula.
Yemen, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Myanmar na Nigeria sasa zinachukuliwa kuwa za wasiwasi mkubwa na zinahitaji uangalizi wa haraka ili kuokoa maisha. Ripoti hiyo pia imetaja Burkina Faso, Chad, Somalia na Syria kama maeneo mengine yenye joto yanayohitaji uangalizi.
Mkuu wa WFP Cindy McCain anasema, "Uwekezaji wa haraka na endelevu katika usaidizi wa chakula na usaidizi ni muhimu katika kuepusha njaa mbaya zaidi inayokaribia."
Katika nusu ya 2025, Umoja wa Mataifa umepokea dola bilioni 5.6 tu, kati ya bilioni 44 zilizopangiwa awali kwa mwaka huu. Tangu Rais wa Marekani Donald Trump arejee madarakani mwezi Januari, Marekani -- mfadhili mkuu duniani -- imepunguza kwa kiasi kikubwa misaada ya kigeni, na kusababisha hali mbaya katika sekta ya kibinadamu duniani kote.
"Hapo awali Washington ilitoa ufadhili wa zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya shirika la UNHCR ambayo ni dola bilioni 2 kwa mwaka”, alieleza mkuu wa shirika hilo Filippo Grandi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili. "Kwa kuzingatia hali ngumu ya kifedha, UNHCR inalazimika kupunguza kiwango cha jumla cha shughuli zake," Grandi alisema katika taarifa ya Jumatatu.