Urusi yabebeshwa lawama ya kuidungua ndege ya Malaysia MH17
13 Mei 2025Ripoti ya Baraza hilo iliyotolewa Jumanne, imebainisha kuwa ndege ya abiria aina ya Boeing 777 iliyokuwa ikielekea Kuala Lumpur kutoka Amsterdam ilidunguliwa kwa kombora la Buk lililotoka katika eneo la Ukraine lililokuwa chini ya waasi wanaounga mkono Urusi.
Uchunguzi wa kimataifa ulioongozwa na Uholanzi mwaka 2016 ulithibitisha kuwa silaha hiyo ya kivita ilipelekwa na Urusi, ingawa Moscow imeendelea kukanusha kuhusika kwake.
Serikali za Uholanzi na Australia ndizo zilizopeleka malalamiko yao rasmi kwa ICAO mnamo mwaka 2022. Tangu awali, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) haikuwa chaguo kwa sababu Urusi haitambui mamlaka ya mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi.
Baraza la ICAO limeamua kwamba Urusi ilikiuka Mkataba wa Chicago wa 1944 unaoongoza sheria za anga za kimataifa, ambao unataka mataifa "kuepuka kutumia silaha dhidi ya ndege za kiraia zilizo angani." Hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kufanya uamuzi wa kipekee katika mzozo baina ya nchi wanachama 193.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Caspar Veldkamp, amesema suala la fidia sasa litajadiliwa na Baraza hilo ndani ya wiki chache. "Tunaomba ICAO iagize Urusi kuanza mazungumzo ya fidia nasi na Australia, na Baraza liwe msimamizi wa mchakato huo ili kuhakikisha kuna nia njema na muda maalum wa utekelezaji," alisema Veldkamp.
Majadiliano ya fidia kwa familia za waathirika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Penny Wong, amepongeza uamuzi huo akisema ni "hatua muhimu ya kihistoria katika harakati za kutafuta ukweli na haki kwa familia za waathiriwa." Amesisitiza kuwa Urusi sasa inapaswa kukiri jukumu lake na kulipa fidia kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Soma pia: Uchunguzi: Putin huenda alitoa Kombora lililoangusha ndege
Hadi sasa, ubalozi wa Urusi nchini Australia haujatoa tamko lolote kuhusu uamuzi huo. Kwa upande wake, mtaalamu wa sheria za kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia, Don Rothwell, amesema ICAO bado haijatoa maelezo ya kina kuhusu sababu za hukumu hiyo. Hata hivyo, anaamini kuwa Baraza hilo litapendekeza Urusi ilipe fidia kwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Tangu ndege hiyo ilipodunguliwa Julai 17, 2014, takriban raia 193 wa Uholanzi, 38 wa Australia, na kadhaa kutoka Malaysia na nchi nyingine walipoteza maisha. Wengi walikuwa na uraia wa mataifa mawili. Wakati huo, Ukraine ililitaja tukio hilo kama "kitendo cha kigaidi," huku waasi wa Ukraine wakidai ilidunguliwa na ndege ya kijeshi ya Ukraine.
Mwaka 2022, mahakama ya Uholanzi iliwahukumu watu watatu kifungo cha maisha kwa kuhusika na tukio hilo, wakiwemo raia wawili wa Urusi. Urusi ilikataa kuwakabidhi watuhumiwa hao. Na mwaka 2023, wachunguzi wa kimataifa walieleza kuwa kulikuwa na "dalili nzito” kuwa Rais Vladimir Putin aliridhia kupelekwa kwa kombora lililotumika.
Kwa sasa, wachunguzi wa kimataifa kutoka Australia, Uholanzi, Malaysia, Ubelgiji na Ukraine wamesimamisha uchunguzi zaidi kwa kukosa ushahidi wa kutosha wa kuwataja washukiwa wengine.
Soma pia:Ni mwaka mmoja tangu ndege ya MH17 kudunguliwa Ukraine
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, amesema uamuzi wa ICAO ni ushindi wa ukweli dhidi ya propaganda. "Haijalishi Urusi imetumia kiasi gani cha fedha kuficha ukweli, haki lazima ishinde," aliandika kupitia ukurasa wa X.
Kwa ujumla, uamuzi huu wa ICAO umeelezwa na mataifa ya Australia na Uholanzi kuwa ni tukio la kihistoria katika kutafuta ukweli, uwajibikaji, na haki kwa wale waliopoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo mbaya zaidi ya anga barani Ulaya katika miongo ya hivi karibuni.