UN: Watu 798 wameuwawa wakisubiri misaada ya GHF Gaza
11 Julai 2025Baada ya vifo vya mamia ya raia waliokuwa wakijaribu kufikia vituo vya misaada vya Gaza Humanitarian Foundation GHF katika maeneo ambayo vikosi vya Israel vinaendesha shughuli zake, Umoja wa Mataifa umeutaja mfumo huo wa utolewaji wa misaada kuwa si 'sio salama'.
Msemaji wa Ofisi ya Haki za BInadamu ya Umoja wa Mataiafa Ravina Shamdasani amesema kuwa tangu Mei 27 hadi Julai 7, wamerekodi vifo 798 vikiwemo 615 karibu na vituo vya misaada vya GHF na 183 wakihofiwa kuuwawa wakiwa njiani kuelekea kwenye vituo hivyo vya misaada.
Aidha Shamdasani amesema kuwa walipokea taarifa pia za majeruhi wengi waliopigwa risasi karibu na vituo vya usambazaji wa misaada tangu Mei 27, na kuonesha wasiwasi wao juu ya uwezekano wa uhalifu mkubwa wa kivita na hatari ya kuendelea kwa uhalifu huo katika wakati ambapo watu wanalazimika kujipanga msururu kwa ajili ya kupata mahitaji ya kimsingi kama chakula na dawa.
"Tumeona katika idadi ya vifo huko Gaza wengi ni wanawake na watoto. Hilo linaibua maswali juu ya kuheshimiwa kwa kanuni za kimataifa za kivita."
Shamdasani aliongeza kuwa "tumeeleza wasiwasi wetu kujusu uhalifu mkubwa wa kivita ambao huenda tayari umetendwa, na hatari ya kuendelea kutendwa kwa uhalifu huo zaidi.
Israel imesisitiza kuwa majeshi yake huendesha oparesheni karibu na vituo vya misaada ili kuzuia misaada kuangukia mikononi mwa wanamgambo wa Hamas.
GHF imesema mapema leo kwamba tayari imesambaza zaidi ya milo milioni 70 kwa Wapalestina wenye njaa ndani ya wiki tano, na kwamba mashirika mengine ya misaada karibu yote yaliokuwa yakiendesha shughuli zake Gaza 'yaliporwa misaada yao' na Hamas au magenge ya kihalifu.
EU: TUnalaani vikwazo vya Marekani kwa Albanese
Umoja wa Ulaya umelaani vikali uamuzi wa Marekani kumuwekea vikwazo mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu katika maeneo ya Palestina Francesca Albanese.
Waziri wa Mambo ya Nje Marekani Marco Rubio, alisema Albanese amekuwa akichochea mashitaka yasiyo halali dhidi ya Waisraeli katika mahakama ya ICC.
Mtaalamu huyo wa Umoja wa mataifa amekuwa mkosoaji mkubwa wa Israel na alitoa ripoti inayozitaja kampuni zaidi ya 60, ikiwemo za Marekani, kwa kuunga mkono makazi ya walowezi na mashambulizi yanyoendelea Gaza.
Wakati hayo yakiendelea Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amehitimisha ziara yake nchini Marekani, bila ya kuwa na mafanikio ya wazi katika mpango wa kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza.