UN: Kundi la M23 limeua watu 169 mashariki mwa DRC
31 Julai 2025Katika moja ya matukio mabaya zaidi ya umwagaji damu tangu kurejea kwa nguvu kwa waasi wa M23, shirika la Umoja wa Mataifa limefichua kuwa takriban raia 169 waliuawa mapema mwezi huu katika shambulio la kundi hilo dhidi ya wakulima na raia wengine mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO), mauaji hayo yalifanyika katika eneo la Rutshuru, mkoa wa Kivu Kaskazini, kuanzia Julai 9.
Taarifa ya UNJHRO inaeleza kuwa waathirika wengi walikuwa wakulima wa jamii ya Kihutu waliokuwa wakijishughulisha na kilimo wakati wa msimu wa kulima.
"Raia, hasa wakulima waliokuwa wakipiga kambi mashambani kwa ajili ya shughuli za kilimo, walishambuliwa. Idadi ya vifo imefikia angalau watu 169," ilisema UNJHRO. Waathirika walikuwa mbali na msaada wowote wa haraka, jambo lililoongeza ukubwa wa janga hilo.
M23 yadai ripoti hiyo ni "kampeni ya udanganyifu"
Kiongozi wa M23 Bertrand Bisimwa amepinga vikali ripoti hiyo na kuahidi kuwa kundi hilo litaanzisha uchunguzi wake wa ndani kuhusu madai hayo.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Bisimwa alisema, "Kabla ya kuweka vikwazo, ukweli wa mambo unapaswa kuthibitishwa kupitia uchunguzi wa kina. Kuchapisha taarifa ambazo hazijathibitishwa ni sawa na propaganda inayolenga kulichafua jina la M23.”
Mashambulizi ya M23 yalielekezwa dhidi ya watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la FDLR, ambalo linaundwa na masalia ya jeshi la zamani la Rwanda na wanamgambo walioshiriki mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Hata hivyo, wanaharakati wa eneo hilo wanasema kuwa waathirika walikuwa raia wa kawaida waliorejea mashambani baada ya M23 kuahidi usalama, hali inayoonesha kuvunjika kwa imani.
Mapambano kati ya M23 na jeshi la Congo yamesababisha vifo vya maelfu na kuwalazimisha mamia ya maelfu kukimbia makazi yao.
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haqq alisema katikati ya mwezi huu kuwa vurugu hizo zimewalazimu washirika wengi kupunguza shughuli zao Kongo Mashariki na hivyo kuyaweka hatarini zaidi maisha ya watu.
"Washirika wa ndani wanasema kuwa mapigano yamesababisha angalau watu 37,000 kuyakimbia makazi yao. Wakati huo huo, katika vijiji vilivyoko mpakani mwa majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, mashambulizi ya makundi yenye silaha ya ADF yanaripotiwa kuua angalau raia 65, huku kadhaa wakijeruhiwa. Wengine wengi bado hawajulikani walipo. Kumeripotiwa uhamishaji wa idadi kubwa ya watu kuelekea maeneo ya Beni na Mambasa."
Ripoti ya wataalamu wa umoja huo iliyotolewa mwezi huu inasema Rwanda inatoa msaada wa kijeshi kwa M23, ikiwa ni pamoja na silaha na uongozi wa moja kwa moja wa kijeshi, kwa lengo la kudhibiti maeneo mashariki mwa DRC. Rwanda imeendelea kukanusha shutuma hizo, ikisema kuwa inalinda usalama wake dhidi ya vitisho vya FDLR na makundi mengine yenye uhusiano na mauaji ya kimbari.
Msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya, amesema mauaji ya Rutshuru ni ushahidi kuwa kundi la M23 haliwezi kuleta utulivu wowote. "Serikali ya Kinshasa inahitaji makubaliano ya amani yatakayorudisha mamlaka kamili ya serikali katika maeneo haya,” alisema Muyaya.