UN: Viwango vya haki za binaadamu vimeporomoka kote duniani
24 Februari 2025Viongozi hao wamepaza sauti kuhusu kuporomoka kwa viwango vya haki za binaadamu kote ulimwenguni. Wamesema mfumo wa ulinzi wa kimataifa ulioundwa baada ya Vita vya Pili vya dunia haujawahi kukabiliwa na changamoto kubwa kama wakati huu.
Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema haki za binadamu zinakandamizwa kote duniani kutokana na migogoro ya kisiasa, hali ya hewa, madikteta, watu wanaochochea vita pamoja na mfumo wa kifedha wa kimataifa usio na maadili ambao umekuwa ukizuia usawa na maendeleo endelevu.
Aidha Guterres ameelezea umuhimu wa kuheshimu haki za binaadamu:
" Bila kuheshimu haki za binadamu, za kiraia, kitamaduni, kiuchumi, kisiasa na kijamii, amani endelevu itakuwa ni ndoto tu. Migogoro inasababisha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kiwango kikubwa."
Guterres amesisitiza kuwa kwa sasa dunia inashuhudia kudorora kwa haki za binadamu, jambo linaloashiria hatua mbaya, huku akiutaja mzozo wa Ukraine uliotimiza miaka mitatu leo na pia ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia: Guterres: Haki za binaadamu zimekandamizwa mno na watawala wa kiimla
Waziri mkuu wa Kongo Judith Suminwa Tuluka ameuhutubia pia mkutano huo wa ngazi ya juu wa Baraza la Haki za Binaadamu na kusema kuanzia Januari mwaka huu, takriban watu 7,000 wameuawa huku wengine 450,0000 wakiwa hawana makazi kufuatia mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC.
Waziri Mkuu huyo wa Kongo amehimiza ulimwengu kuchukua hatua na kutangaza vikwazo kwa wahusika. Bi Suminwa ameongeza kuwa mayowe na vilio vya mamilioni ya wahanga wa mzozo huo hayaelezeki.
Kauli ya Kamishna Mkuu wa haki wa Umoja wa Mataifa
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ametahadharisha kuwa ulimwengu uko hatarini kurejea kwenye zama za utawala wa kibabe akisisitiza kuwa watawala wa kimabavu sasa wanadhibiti karibu theluthi moja ya uchumi wa dunia ikiwa ni idadi mara mbili ukilinganisha na kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Turk amesisitiza kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa mamlaka za kikanda ambazo amesema zinaonekana kutoshughulishwa na uheshimishwaji wa haki za binadamu.
Philemon Yang, Mwenyekiti wa kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema katika mkutano huo kuwa kudorora kwa haki za binaadamu kunatokana na kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji na kupuuzwa kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ukiukaji ambao una madhara makubwa.
Yang ameongeza kuwa wahathiriwa mara nyingi ni wanawake, watoto na watu wa jamii za walio wachache. Kiongozi huyo amehitimisha kuwa vitendo vya mateso na uharibifu wa miundombinu vinavyoshuhudiwa huko Gaza, Ukraine, Sudan, Myanmar, Haiti na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni lazima vikomeshwe.
(Vyanzo: Mashirika)