UN:Vifo vya raia katika mashambuzi ya Darfur vyapindukia 300
15 Aprili 2025Takriban raia 300 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya siku mbili yaliyotekelezwa na kikundi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) katika kambi za wakimbizi wa ndani huko Darfur Kaskazini, Sudan.
Umoja wa Mataifa kupitia ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) umethibitisha taarifa hizo kwa kuzingatia vyanzo vya ndani, ukionya kuwa huenda idadi hiyo ni kubwa zaidi kutokana na hali duni ya mawasiliano na usalama.
Soma pia: RSF yazidisha mashambulizi, vita vya Sudan vikifikisha miaka miwili
Mashambulizi hayo yaliyolenga kambi za Zamzam na Abu Shorouk, pamoja na mji mkuu wa Darfur Kaskazini – El Fasher – yamekuja baada ya jeshi la Sudan kudhibiti upya mji wa Khartoum, ushindi muhimu katika vita ambavyo vimeendelea kwa karibu miaka miwili sasa.
Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa, watoto 20 na wafanyakazi wa misaada tisa ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo.
Tangu kuzuka kwa mzozo huo mnamo Aprili 2023, Sudan imekumbwa na moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku ikiorodheshwa kuwa nchi pekee kwa sasa inayokumbwa na baa rasmi la njaa. Viongozi wa kimataifa wanatoa wito wa msaada wa dharura na usitishaji wa mapigano ili kuokoa maisha ya mamilioni walioko hatarini.