UN: Maafisa Myanmar waripotiwa kuwatesa raia wake
12 Agosti 2025Shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia katika uchunguzi wa uhalifu Myanmar (IIIM) lililoundwa mwaka 2018 kutambua na kuchunguza ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, limesema baadhi ya mateso kwa waathirika ni pamoja na kupigwa vibaya, kuchomwa na nyaya za umeme, kunyongwa na aina nyengine ya mateso kama kun'golewa kucha kwa kutumia koleo.
Kulingana na Mkuu wa shirika hilo Nicholas Koumjian, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ilio na kurasa 16 inaelezea mateso ya watu wa Myanmar, ambayo wakati mwengine yalisababisha vifo. Watoto waliokamatwa pia walipitia mateso hayo.
Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi ya jeshi la Myanmar
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya kijeshi ya Mnyamar hakupatikana kutoa maoni yake juu ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa. Serikali hiyo haijawahi kutoa maoni juu ya ripoti zote zilizotolewa na umoja huo kuhusu madai ya uhalifu na ombi pia la kutaka wachunguzi hao kuingia nchini humo.
Mara zote jeshi limekuwa likikanusha kuwatesa raia likidai magaidi ndio wanaozua hali ya sintofahamu nchini humo, huku likisisitiza kuendelea kusimamia jukumu lake kuhakikisha uwepo wa amani na usalama Myanmar.