UN: Kuna hatari ya baa la njaa Sudan
13 Juni 2025Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuhusu hatari ya kuzuka baa la njaa na kukosekana ulinzi kwa raia, huku mkuu wa huduma za kiutu wa Umoja wa Mataifa akiilaumu dunia kwa kunyamaa kimya.
Sudan imegeuka na kuwa mfano wa kusikitisha wa dunia iliyokosa hisia na kutojali, huku kukikosekana uwajibikaji na kuruhusu mauaji, njaa na mateso yakienea kwa kasi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, aliyetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kuwalinda raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika kote nchini Sudan.
Nusu ya idadi ya watu wanahitaji msaada wa chakula
Kwa mujibu wa Fletcher, nusu ya idadi ya watu wa Sudan, takribani milioni 30, wanahitaji msaada wa dharura kuokoa maisha yao, katika kile anachokielezea kuwa "janga kubwa kabisa la kibinadamu duniani kwa sasa.” Kero yake ni kwamba licha ya ahadi nyingi za kimataifa, vita vinaendelea, raia wanaendelea kuuawa, wanajeruhiwa na wanapoteza mali na makazi yao.
Katika mkondo mpya wa vita, kikosi cha wanamgambo wa RSF, kimedai kuliteka eneo muhimu la mipakani kati ya Sudan, Libya na Misri, ambalo ni "eneo lenye umuhimu mkubwa wa biashara na usafirishaji wa mafuta na madini.”
Hatua hiyo imeongeza wasiwasi wa vita kupanuka zaidi, baada ya jeshi la Sudan kudai kuwa vikosi vya Kamanda wa Libya, Khalifa Haftar, vimeunga mkono mashambulizi ya RSF, madai ambayo Libya imeyakanusha.
Mapigano haya mapya yanatokea wakati ambapo maeneo kadhaa kusini mwa jiji la Khartoum yanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP, limetahadharisha kwamba "uhaba wa chakula cha msaada ” unaathiri mamilioni ya watu waliokwama katika maeneo ya vita. Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Laurent Bukera ametoa tamko linalochora taaswira ya hali ilivyo.
"Mahitaji ni makubwa mno. Tumeshuhudia uharibifu mkubwa, ukosefu wa maji, huduma za afya, umeme, na milipuko ya kipindupindu. Katika baadhi ya maeneo maisha ya kawaida yanarejea polepole, lakini mengine yamebaki kama miji ya mizuka. Katika miezi sita iliyopita, tumefanikisha kuwafikia takribani watu milioni moja mjini Khartoum kwa msaada wa chakula na lishe," alisema Bukera.
WFP imesema mgao wa chakula umepunguzwa hadi asilimia 70 ya kiwango cha kawaida, kutokana na upungufu wa ufadhili wa zaidi ya dola milioni 500. Tayari maeneo kama Jebel Awlia yameripotiwa kukabiliwa na hali ya njaa kali.
Watu 24,000 wamefariki dunia
Kwa upande wa kijeshi, mji wa El-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, umekuwa kitovu kipya cha mapigano makali — ukiwa ndio mji wa mwisho katika eneo la Darfur ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la serikali,huku RSF ikiendeleza mashambulizi ya maroketi na mashambulizi ya droni katika miji iliyobaki chini ya jeshi.
Vita hivi, vilivyoanza mwezi Aprili mwaka 2023, vimesababisha hadi sasa vifo vya takriban watu 24,000, ingawa huenda idadi ikawa ni kubwa zaidi, na kuwalazimisha watu milioni 13 kuyakimbia makazi yao, wakiwemo milioni 4 waliokimbilia nchi jirani.
Mauaji ya halaiki, ubakaji wa wanawake na mauaji ya kikabila, hasa katika Darfur, vimetajwa kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Hadi sasa, juhudi za kidiplomasia za kimataifa kusitisha mapigano hayo zimegonga mwamba, huku mapigano yakizidi kuenea katika maeneo ya Darfur na Kordofan. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa bila msaada wa haraka na hatua madhubuti, Sudan inasalia kuwa janga linalokodolewa tu macho na jamii ya kimataifa — kwani dunia imekosa kuchukua hatua stahiki.