Hali Sudan Kusini inazidi kuzorota kwa kiwango cha kutisha
9 Machi 2025Taarifa hiyo imetolewa Jumamosi siku kadhaa baada ya washirika kadhaa wa makamu wa Rais wa taifa hilo, Riek Machar kukamatwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Yasmin Sooka, ametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kuzingatia tena haraka mchakato wa amani, kuheshimu haki za binadamu na kuhakikisha hakuna vikwazo kuelekea kwenye demokrasia.
Soma pia: Helikopta ya Umoja wa Mataifa yashambuliwa Sudan Kusini
Mwanzoni mwa mwezi wa Machi vikosi tiifu kwa Rais Salva Kiir viliwakamata mawaziri wawili na maafisa kadhaa wa ngazi ya juu wa jeshi ambao ni washirika wa Riek Machar.
Hali hiyo imezua hofu juu ya mustakabali wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018, yaliyovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitano vilikuwa kati ya vikosi tiifu kwa Riek Machar na Salva Kiir na watu karibu 400,000 waliuwawa.