EU yapongeza makubaliano kati ya Armenia na Azerbaijan
9 Agosti 2025Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Antonio Costa na mwenzake anayeongoza Halmashauri Kuu ya Umoja huo Ursula von der Leyen wamesema makubalino hayo yanapaswa kuanza kutekelezwa haraka.
Mpango huo wa amani umesimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump aliyewakaribisha jana katika Ikulu ya White House Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev. Trump amesema pande zote zimeafikiana kusitisha kabisa mapigano, kuanzisha uhusiano kidiplomasia, biashara, usafiri na kuheshimu uhuru na mipaka ya kila mmoja.
Armenia yenye Wakristo wengi na Azerbajan yenye Waislamu wengi kwa muda mrefu wamekuwa wakizozania eneo la Nagorno Karabakh na waliingia vitani mara mbili. Azerbajan ilichukua udhibiti wa eneo hilo katika shambulio la mwaka 2023, na kupelekea zaidi ya Waarmenia 100,000 kuyahama makazi yao.