EU yapendekeza sheria kuharakisha kuwaondoa wahamiaji
11 Machi 2025Tume ya Umoja wa Ulaya imependekeza sheria mpya zinazolenga kuufanya mchakato wa kuwarejesha makwao wahamiaji kuwa na ufanisi. Moja ya yaliyopendekezwa ni kuwawekea vikwazo vya kifedha waomba hifadhi wasiotoa ushirikiano kwa mamlaka.
Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Magnus Brunner amesema katika mfumo mpya wa Umoja wa Ulaya wa kuwarudisha wahamiaji, umoja huo utahakikisha kuwa wale wasio na haki ya kuishi katika nchi wanachama wanaondolewa.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya wajizatiti zaidi juu ya wahamiaji haramu
Ameeleza kuwa mabadiliko yanayopendekezwa yataimarisha uaminifu katika mfumo wa pamoja wa uhamiaji wa Ulaya wa kuomba hifadhi barani Ulaya. Kulingana na Tume ya Umoja wa Ulaya, kwa sasa ni asilimia 20 pekee ya wahamiaji wanaoamriwa kuondoka Ulaya ndiyo wanaorudi walikotoka. Wengi wa wahamiaji waliokataliwa maombi hayo husalia katika nchi husika licha ya kukataliwa kwa kuwa mataifa walikofikia awali yanawakataa au yanachukua muda mrefu kuchukua hatua.
Brunner amesema Umoja wa Ulaya utaziruhusu nchi 27 wanachama kuanzisha nje ya umoja huo vituo watakamowekwa wahamiaji wanaotakiwa kurejeshwa makwao.
Maombi ya hifadhi kutoka nchi moja kupelekwa moja kwa moja kwa wanachama wengine
Katika sheria hiyo maombi ya kuwaondoa wahamiaji kutoka nchi moja ya Umoja wa Ulaya yatapelekwa moja kwa moja na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya. Chini ya sheria mpya inayopendekezwa hairuhusiwi kwa nchi moja kukamilisha mchakato wa maombi ya hifadhi na kwa mchakato mwingine kuanzishwa katika taifa jingine la umoja huo.
Mabadiliko hayo yanayopendekezwa ya sheria ya uhamiaji yametokana na mjadala wa umma unaozidi kushika kasi kuhusu suala hilo ambalo limesababisha vyama vya mrengo wa kulia kuzidi kuungwa mkono kwenye chaguzi katika nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya. Hilo limeongeza shinikizo kwa serikali za umoja huo kuongeza makali katika misimamo yao juu ya waomba hifadhi na wahamiaji wasio na vibali.
Mnamo mwezi Oktoba, viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiongozwa na nchi zenye misimamo mikali dhidi ya uhamiaji zikiwemo Sweden, Italia, Denmark na Uholanzi, walitoa wito wa kuundwa kwa sheria mpya ya kuharakisha kuwarejesha makwao wahamiaji wasiofuata sheria. Walitaka pia tume ya Ulaya itathmini njia zenye ubunifu za kupambana na uhamiaji haramu.