Umoja wa Ulaya waongeza vikwazo vipya Urusi
18 Julai 2025Vikwazo hivyo vinakusudia kupunguza zaidi mapato ya Urusi kutokana na mauzo ya mafuta kwa nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya, na pia kuathiri sekta ya kifedha ya Urusi.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema wataendelea kuongeza mbinyo hadi pale Urusi itakapositisha vita dhidi ya Ukraine.
Slovakia ilikuwa kizuizi kikuu cha makubaliano haya, ambapo Waziri Mkuu Robert Fico alitishia kutumia kura ya turufu, lakini hatimaye makubaliano yalifikiwa baada ya Slovakia kupewa hakikisho kuwa haitapata athari kubwa za kiuchumi endapo Umoja wa Ulaya utaamua kusitisha kabisa uagizaji wa gesi kutoka Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amepongeza duru mpya ya vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi akivitaja kuwa "muhimu na vilivyokuja katika wakati muafaka.”