Umoja wa Ulaya kuzungumza na uongozi wa China Alhamis
24 Julai 2025Mazungumzo hayo yatajikita katika msuguano uliopo katika masuala ya kibiashara na hata vita vya Ukraine, huku kukiwa na matumaini finyu ya kupatikana kwa suluhu.
Kanda za video za mashirika ya habari ya China zimewaonesha Von der Leyen pamoja na Costa wakiwasili katika mji huo mkuu wa China wakiandamana na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas.
Wakuu hao wa Umoja wa Ulaya watafanya mkutano na Rais Xi Jinping pamoja na Waziri Mkuu Li Qiang.
Brussels inasema mkutano huo ni fursa ya wazi ya hatua za kina na muhimu kuchukuliwa katika masuala yote katika mahusiano yao na China.
Beijing imeamua kuusogeza karibu Umoja wa Ulaya, huku ikijitanabahisha kama mshirika wa kutegemewa zaidi kuliko Marekani na mwamba wa uthabiti katika dunia yenye matatizo chungunzima.